Tunauanza mwaka mwingine kwa bahati tu, tulianza nao wengi na wengine nusura tumalize nao lakini haikuwa hivyo. Si kwamba hawakuwa na nguvu, la hasha! Si kwamba hawakuwa na madaraka, la hasha! Vilevile si kwamba hawakuwa wajanja, bali neno lilitimia juu yao na kutwaliwa kwa wakati wao.

Najiuliza maswali mengi, kwanini sikuwa mimi na kwanini mimi niliachwa kwa mwaka mzima huku wenzangu wakitwaliwa na wengine wakiwa hospitalini kwa mwaka mzima? Ni kwa sababu kazi ambayo amenipatia labda sijaimaliza na pengine kusudio lake halijatimia juu yangu. Uwepo wako mpaka leo ni kwa sababu hizo.

Leo ninaandika waraka huu kukutaka msomaji wangu kujua kwamba tunamhitaji zaidi Mungu katika kipindi hiki ambacho tumezingirwa na mambo mengi ya hatari kuliko wakati mwingine wowote wa kizazi hiki kumhitaji Mwenyezi Mungu.

Kipindi hiki ni cha hatari ambazo ni lazima tukumbushane kama binadamu, ni kipindi ambacho hata imani potofu zimetuandama kuliko wakati wowote. Ni kipindi ambacho binadamu mwenzetu ameaminishwa kwamba binadamu mwenzake ni kitoweo na leseni ya mafanikio ya maisha.

Kipindi hiki ni cha hatari kwa maradhi ambayo sisi wengine ambao hatukuishi leo, bali tangu zamani tunaona kila kitu ni sumu. Ni kipindi ambacho maradhi mapya ya hatari yanaibuka na kutupoteza katika sura ya dunia kwa sababu ambazo kila mtu anashindwa kujua nini hatima yake.

Kipindi hiki ni kibaya kwa imani zetu, uhusiano wetu na Mungu unaingiliwa na binadamu wenzetu katika kutupotosha mawasiliano yetu tuliyokuwa nayo. Imani mbalimbali zimepandwa katika mioyo yetu kiasi cha kutufanya tuwe mbali na imani za kweli. Tunaishi kinyume cha vitabu vitakatifu na kuaminishwa miungu ya duniani ambayo inatupotosha.

Kipindi hiki ni kigumu kwa sababu ya tamaa za wenzetu wachache wenye uwezo wa kutushawishi tuwaamini kisiasa huku wakijua kwamba wanaturubuni ili matumbo yao yaweze kushiba na kusaza, ni kipindi cha kushawishiwa kukataa mamlaka za duniani ili kuamini mamlaka bandia ambazo zinataka dola kwa kututumia na wakati mwingine tunamwaga damu zetu kwa kuaminishwa.

Najua kwamba mabadiliko ni lazima yaje, lakini ni mabadiliko gani ndilo swali la msingi. Na je, mabadiliko hayo lazima yaje na hatari kwa viumbe vya Mwenyezi Mungu na hata kubadili namna ya maisha yetu? Ni kweli kwamba maendeleo ya leo ili yapatikane ni lazima tukengeuke katika maadili na vitabu vya dini? Je, tunahitaji msaada wa binadamu katika ulinzi badala ya Muumba?

Waraka huu ninataka tujitafakari tu, tulikuwa wapi na tupo wapi. Ninataka tujiulize kama ni kweli upendo wa Mungu bado upo au umepotea? Je, ni kweli kwamba maisha tunayoishi yanampendeza Mungu kwa maana ya kuishi kama ambavyo alipenda tuishi?

Nadhani hiki ni kipindi ambacho tunamhitaji Mungu zaidi kuliko wakati wowote ule, kwa sababu nyingi sana, tunaona mabadiliko ya tabia nchi, uamuzi wa watu wachache kujilipua kwa imani potofu, watu wachache kusema wametumwa na Mungu kuja kutukomboa kwa kufanya mambo kinyume cha kitabu kitakatifu.

Kipindi hiki ni cha tamaa na wivu uliopitiliza, ni kipindi cha Sodoma na Gomora, ni kipindi cha hatari ya kila kitu, iwe chakula, dawa, hewa, mavazi na vitu vyote. Ni kipindi cha malezi ya upande mmoja, ni kipindi cha kubadili jinsia zetu, ni kipindi cha haki za uongo kutamalaki duniani.

Kuna mambo mengi sana ninayoyaona kwamba yanahitaji msaada wa Mungu kuliko wakati mwingine wowote tulioishi. Mambo ni mengi na yanatubadilisha kila siku kutokana na watu wachache kutumia fursa ya shida zetu katika kutatua matatizo yao.

Tumrudie Mungu kama familia na tufike mahali tufanye hivyo kama taifa. Tufanye toba kwa ajili ya taifa letu. Taifa ni la Mungu na anaweza kuamua kutusikiliza iwapo tutapita katika njia nyoofu.  Tujiulize maswali mengi yahusuyo maisha yetu kuliko kuwa na majibu machache kuhusu maisha yetu, na hasa katika kipindi hiki kiitwacho cha maendeleo ya teknolojia.

Niwatakie afya njema na tafakuri nzito kwa mustakabali wa maisha yetu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri