Nataka niwe mtu wa tatu kupigana na utaratibu wa maisha ya Mtanzania kuwekewa mazingira ya kifo ambayo hakustahili, mazingira haya yanatayarishwa bila mtayarishaji na anayetayarishiwa kujua kuwa anaandaliwa mazingira ya kifo.

Miezi kadhaa iliyopita, nilipata kuzungumzia adha ya pikipiki ambayo kwa mujibu wa kikao chetu cha Bunge, kiliazimia kwa kauli moja kufuta kodi ili kuongeza ajira kwa vijana, inaweza ikawa ndiyo ile ahadi ya ajira milioni moja.

Wiki jana katika safu ya Sitanii, mwenzangu alijaribu kuzungumzia athari za ajira hii mpya, ambayo imevuruga utaratibu mzima wa sheria na amani nchini, lakini zaidi ya hapo imeongeza idadi ya vifo na ulemavu usioweza kuvumilika kwa mtu yeyote mwenye akili timamu.

Kuna hoja za kijinga ambazo zinatolewa na watu wengi kuwa mataifa yote yaliyoendelea yanatumia usafiri wa baiskeli na pikipiki. Watoa hoja wamesahau kuwa wenzetu wametangulia katika suala la sheria na utii, wametangulia katika nidhamu na elimu ya matumizi ya vifaa hivyo.

Nilipotoa maoni yangu kuhusu adha ya usafiri wa pikipiki na suala la kufuata sheria, baadhi ya wadau walionesha kukubaliana nami, sikutaka kupingana na hoja ya ajira kama ilivyokusudiwa na waliofikiria lakini nilitaka wafike mbali zaidi, tuione ajira hiyo kama zilivyo ajira nyingine za udaktari na uhasibu.

Wanaopakiwa wanaamini kuwa madereva wao wamefuzu masomo hayo ya kusafirisha abiria, lakini matokeo yake linapotokea jambo la hatari anayeanza kukimbia ni dereva na abiria anabaki akijiuguza kama si kukutana na kifo. Tunawapa madaktari wakati mgumu wa kutibu majeruhi zaidi kuliko wagonjwa wengine kwa uzembe wa ajira ya bodaboda.

Tunaligharimu Taifa dawa, damu, wataalamu na viungo bandia wakati tungeliweza kupingana na athari hizo kwa kutumia wasomi wetu wanaoweza kupembua mambo na kuona athari kubwa zaidi inayoweza kuja mbele yetu.

Kwa maoni yangu ya wakati ule nilisema ni vema tukatoa mafunzo kwanza kwa hao wahitaji wa ajira hizo na si kufanya biashara ya zimamoto bila kuangalia athari zake. Nilisema pia ni vema adhabu zinazotakiwa kutolewa zikaangaliwa upya ili kuweza kudhibiti makosa ambayo yanajitokeza mara kwa mara.

Wanaoumia na matumizi ya hii ajira mpya ambayo kwangu mimi sijui kama ni mpango wa chama chochote ama kikundi fulani ni watoto wetu, wazazi wetu, vijana wa Taifa la kesho na nguvu kazi tunayoitegemea miaka kadhaa ijayo.

Pia nilishauri kuwa kutokana na wimbi kubwa la ajali ambazo zinatokea kwa uzembe wa madereva wote wawe wa pikipiki au magari, ni vema tukajipanga katika kukusanya mapato makubwa na kufanya mambo ya maendeleo. Niliwalaumu askari wa usalama barabarani kwa kutokusanya mapato kama wale wenzao wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Zinaweza kuwa hoja za kijinga lakini mliofikiria kuwa pikipiki ni sehemu ya ajira naomba mfikirie upya na muangalie athari zake, vinginevyo nitaamini kuwa nchi yetu ni ya kutayarishiana mazingira ya kifo na hao wenye nguvu ya utawala.

Pia nimejaribu kuangalia mtazamo uliopo wa dawa za kulevya na hadithi tamu zinazotolewa hao wenye nguvu ya kuweza kuzuia biashara hii ambayo si haramu hapa Tanzania. Taifa linaelekea kuteketea nguvu kazi kwa maslahi ya watu wachache kujinufaisha kwa muda mfupi.

Kuna taarifa mbalimbali ambazo zinatolewa na wahusika na dawa hizo, zimeandikwa barua katika mitandao ya jamii, zimetolewa taarifa kwa vyombo vya habari, Watanzania kadhaa wameshikwa katika mataifa mengi nje na tunashindwa kuchukua hatua, tunakuwa na kigugumizi cha kupambana na wafanyabiashara hawa.

Enzi zetu tulipata kuwa na tatizo la watu wavivu, ilianzishwa operesheni ya kuwataja hadharani na wakachukuliwa hatua, pia kuna wakati tulikuwa na wimbi la majambazi tukapiga kura za siri wote wakakamatwa. Huo moyo wa uzalendo uko wapi katika kizazi hiki?

Viongozi mlioko madarakani mngelipenda kuongoza akina nani baada ya miaka ishirini, najiuliza mngelipenda kuongoza makaburi yatokanayo na ajali za pikipiki, vilema, vichaa ambao wanatokana na kuathirika kisaikolojia na matatizo ya ndugu zao ama mateja kutokana na dawa za kulevya?

Naamini hakuna kinachoshindikana, na kama kuna kushindwa basi kuna mkono wa mtu mkubwa, naomba tujiulize huyo ni nani? Kwanini atuathiri tulio wengi kwa manufaa yake? Tunalipeleka wapi Taifa hili na hasa kwa wakati huu ambao tunatakiwa kupingana kutokana na uelewa mkubwa uliopo?

 

Wasalaam,    
Mzee Zuzu 
Kipatimo.

 

1217 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!