Nianze waraka wangu kwa kuwapongeza wale wachache, ambao kimsingi wanakubaliana na mabadiliko ya kazi kila siku japokuwa nao ni kama kumkunja samaki aliyeanza kukauka, kuna siku wanaweza kuvunjika wakiwa katika jitihada za kujikunja.

Nchi yetu ipo katika kipindi kigumu cha mabadiliko katika nyanja mbalimbali za kiuwajibikaji, wapo waliodhani mtindo wa ukiritimba ni sehemu ya maisha na sasa kufanya mambo bila ukiritimba ni kama kikwazo kikubwa kwao na hao waliokuwa wanasaidia kuongeza ugumu wa mambo ili waweze kupata mavuno katikati ya majukumu.
Katika kipindi hiki ndipo tunapoona urahisi wa mambo mengi na pengine kuokoa muda kwa mambo ambayo awali tulikuwa tunaweza kutumia muda mrefu kusubili utekelezaji wake, napongeza maeneo yote ambayo yameamua kwa kauli moja kubadilika.

Katika kipindi hiki cha mabadiliko ndiyo tunagundua umuhimu wa teknolojia za urahisishaji mambo, teknolojia ambazo wenzetu walioendelea walizitumia na kufika hapo walipo, hizi ni teknolojia ambazo zilikuja kwa nia ya kurahisisha katika kipindi hicho baadhi yetu waliona ni kama komoa ya ulaji wao na hivyo kuamua kuzitupilia mbali.
Yapo maeneo mengi sana ambayo naweza nikayazungumzia, lakini nichague machache na yale kielelezo hayo mengi na athari zake ambazo zinajitokeza na lengo la  kukwamisha matumizi ya teknolojia. Kuna wakati kulikuwa na tatizo la viingilio vya soka katika viwanja vyetu vya burudani, mapato yalikuwa hayaonekani kwa wenye vyama vyao.
Uamuzi wa kuamua kutumia teknolojia ya kukata tiketi kwa njia rahisi zaidi na isiyogharimu zaidi ilianza kupigwa vita na wale wachache na kutengenezwa mizengwe ya kuonesha kwamba jambo hilo haliwezekani na ni hasara kubwa kwa wanachama  wanaotaka kuona faida ya fedha ipatikanayo.
Hali hii imelikumba kundi kubwa ambalo kimsingi lilikuwa likiishi kwa ukiritima huu, tumeanza kuona malalamiko kutoka kwa wachache na jinsi ambavyo tukitumia teknolojia sisi wanufaika tunaona mambo yakienda vema na haki pasi na kupoteza muda.

Huo ni mfano mmoja tu, lakini ukiangalia katika mambo mengi katika tasnia mbalimbali ndipo utajua athari kubwa ya kumkunja samaki ili akubali kwenda matakwa ya mhitaji, mathalani mambo ya ardhi yalivyokuwa kizungumkuti na yalivyo kizungumkuti pamoja na jitihada zinazoendelea kulikwamua tatizo hilo kila siku.
Tujaribu kufikiria hali ilivyokuwa ngumu ya kupata huduma ya umeme miaka michache iliyopita na hasa wakati ule wa kuhitaji mita ya umeme na mfungaji umeme katika nyumba ambayo umeijenga, fikiria lile kundi la vijana waliokuwa wakikupokea hapo ofisini na mbwembwe zao za kukutoa mlungula ili usilale na giza, napongeza jitihada ambazo zinaelekea kumaliza tatizo la uhitaji wa mlungula na kuokoa muda.
Kumbukeni matatizo tuliyokuwa tunapata hospitali na ambayo mengine bado yapo yakiendelea kupatikana katika hospitali zetu za Serikali, urasimu katika vipimo na kumuona mganga, urasimu wa kupata dawa na vifaa tiba, kuna mtihani wa kubadilika unatusubiri sana.

Nani anakumbuka matatizo ya mahakamani na haki ya mwananchi mwenyewe kisheria, nani anaweza kushuhudia matatizo aliyopata katika vituo vya polisi, TRA, Serikali za Mitaa, Uhamiaji, Magereza, ofisi za leseni, ofisi za viongozi wa Serikali waandamizi  na kadhalika.
Nani anaweza kuwa shahidi na kuwakumbuka baadhi ya miungu-watu ambao walijitengenezea himaya ya kupata malipo pasipo kufanya kazi, nani anakumbuka watu wachache waliokuwa wateule katika tenda mbalimbali kisha kuziuza kwa wengine kwa bei ndogo?
Najua kuwa ni kipindi kigumu kwa wengi hasa tunapolazimika kuzitumia teknolojia na uwezo wetu binafsi kuwasaidia watu wengine kwa kuokoa muda na kutenda kwa ufanisi, ni wakati ambao kila kitu kinatakiwa kufanywa kwa uwazi na haraka ya muda.
Naamini uwajibikaji hautaweza kumwacha mtu huru hasa kama anataka kutoa huduma kwa haki mbele ya walafi wachache ambao wanadhani kujilimbikizia mali ni sehemu ya utamaduni wa kila mtu, tusifanye kila anayeajiriwa afikirie kujinufaisha kwa kuanzisha kaurasimu katika ofisi yake ili apate riziki zaidi ya ile inayotokana na mapato ya umma.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo

828 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!