Kuna wakati huwa nakumbuka hotuba fupi ya aliyewahi kuwa Mheshimiwa Rais wa Uganda enzi hizo, Idi Amin Dada, aliyesema Uganda ina demokrasia ya kuongea utakacho lakini baada ya demokrasia hiyo hujui nini kinachoendelea.

Wengi tulimjua huyu bwana kwa ujuha wake, lakini mimi na wenzangu tulimheshimu kwa kutengeneza mazingira ya kuongoza nchi kwa mabavu.

Neno demokrasia lina maana pana na nzuri sana, lipo katika mukhtadha mpana sana. Ndani ya nyumba kuna demokrasia ya uhusiano, watoto na dada wa kazi, au kaka wa kazi, shuleni kuna demokrasia kati ya walimu na wanafunzi na pia walimu kwa walimu, kazini ni baina ya wafanyakazi na wakubwa, kila mahali kuna demokrasia lakini ni jinsi gani inatumika; hilo ni swali jingine baada ya demokrasia kutumika.

Siku za hivi karibuni, Tanzania tuliridhia mkataba wa vyama vingi vya siasa, maana yake ni kuongeza wigo wa matumizi ya siasa kwa upande wa pili kuweza kushawishi wanachama kuelewa kinachoendelea. Tulipokubali mfumo wa vyama vingi tulikubali kupata changamoto mpya za kisiasa kutoka kwa wenzetu, tulikubali matumizi ya siasa yawepo kwa makubaliano ya yatakayofuata sheria mama za Taifa.

Siku za hivi karibuni, siasa imeshika kasi sana hapa nchini kwa kigezo cha demokrasia, kazi hatufanyi tukiamini siasa ndiyo kazi, katika msingi wa familia tunazungumza siasa, tunabishana masuala ya kisiasa kati ya familia zetu, tuna makundi ya kisiasa hadi katika kaya zetu matokeo yake tunajenga chuki ndani ya familia kwa siasa.

Siasa imevuka mipaka. Ipo katika maeneo yetu ya kazi, tunaweka mafaili pembeni ili kujadili siasa tukiwa katika mwavuli wa demokrasia, tunazima mitambo viwandani ili tujadili siasa, tunaleta mahaba ya siasa sehemu za kazi, wakulima wanafanya siasa mashambani kwa kuwa ni haki yao kidemokrasia, watumishi wa umma hali kadhalika wanapoteza muda wa mwajiri kwa kufanya siasa.

Siasa tukiiacha iendelee kujengeka katika jamii yetu ya kupokea demokrasia kirahisi, kuna siku tutasikia askari wetu wakijadili siasa katika makambi yao ya jeshi, tutasikia makanisa yetu yakifungua mashina ya ukereketwa wa siasa kwa kuwa nayo yanageuka kuwa majukwaa ya siasa badala ya kuabudu.

Uhuru wa kuongea una mipaka na ndiyo maana tunachagua maneno ya kuongea tuwapo na watoto wetu kama wazazi, tunachagua maneno ya kuongea tuwapo na wakwe zetu, tunachagua maneno ya kuongea tukiwa na viongozi wetu, tunachagua maneno ya kuongea tukiwa na wageni. Si kweli kwamba kutokana na uhuru wa kuongea basi tunaweza kusema chochote.

Uhuru wa kuongea unazingatia na muda pia, si kwa sababu kuna uhuru wa kuongea basi unaweza kuongea mahala panapohitaji utulivu, hatuongei kwa sababu tunaweza kuongea ni lazima tuangalie pia tunaongea nini kwa faida ya nani na lini. Iwapo maongezi yako yanaweza kusababisha watu wakachinjana basi hiyo kauli yako si salama kwa wanaokusikiliza.

Uhuru wa kuongea lazima uwe na tija kwa Taifa ambalo tunahangaika na umaskini, katu hatuwezi kujikomboa kwa kuongea, Taifa maskini kama letu demokrasia inatakiwa iwe na mipaka, siamini kuongeza ajira katika siasa ya kuongea.

Idadi kubwa ya wananchi hivi sasa wanaamini katika siasa, wapo radhi kuacha kazi wasikilize siasa, wapo tayari kuacha majembe wakae vijiweni wabishane kuhusu kisiasa, wapo tayari kuacha masomo darasani waandamane kwa ajili ya siasa.

Kabla ya uhuru tulikuwa na vyama vingi, vikaungana na tukawa na chama kimoja ili kiwe na nguvu tuweze kupata uhuru wetu. Moja ya misingi tuliyojiwekea ni pamoja na siasa ni kazi kwa maana ya kwamba siasa bora ni kulima na kufanya kazi na siyo mikutano kama ilivyo leo.

Enzi zetu, siasa ya maneno tulifanya baada ya kazi, tuliongea baada ya kutoka shamba, aliyefanya siasa muda wa kazi alikuwa bepari, hatukumuhitaji katika jamii yetu kwa kuwa hakuwa mshiriki wa kazi za maendeleo.

Ilipo Tanzania ni lazima tufanye kazi, siasa haina nafasi baada ya uchaguzi kwisha, tukumbuke hakuna taifa lililoendelea kwa udalali. Ili tuendelee, tunapaswa kutumia nguvu zetu kwa kufanya kazi na siyo kuongea.

 

Wassalaam, 

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri