Wiki kadhaa zilizopita, niliwahi kuandika hapa juu ya kasumba ya kudharau kilicho chetu na kuona cha watu wengine ni bora kuliko chetu. Niliwakumbusha maisha yetu ya kujitegemea siku chache baada ya Vita ya Uganda jinsi tulivyofunga mikanda na kujitegemea kwa kila kitu, na tuliweza kwa asilimia mia.

Leo nashika kalamu kwa kuwa naona tunaelekea ukingoni katika kasumba ya kuiga mambo. Tulianza kuiga tukiamini ni maendeleo, baada ya kuiga kwa muda tukabaini kuwa mambo mengi tunayoiga yapo katika kumnufaisha tunayemuiga, tuliiga mavazi ikabidi tuwekeze fedha katika mavazi, tukasahau mavazi yetu na tukajipofusha hadi vazi la Taifa tukakosa.

Tukaiga vyakula vyao, tukasahahu kuwa tuna vyakula vyetu vya asili na vyenye virutubisho vingi, tukakataa kula vyetu tukiamini vile vinavyotoka nje ndivyo bora kuliko vya mashambani kwetu. Leo tumefikia mahali tunakula vyakula vya kutoka nje ya nchi bila kujali kama viko salama ama la.

Tukaiga lugha yao, pamoja na matege yote tuliyonayo katika kuongea lugha tuliyoiga, bado tunaoana ni ufahari kuzungumza lugha yao kwa kusuasua na kutomaanisha tunachoongea. Tumefika mahali hatuelewani kwa kutumia lugha ya watu, tumefika mahali tunamthamini anayetumia lugha ya watu, tumefika mahali watu wanakufa kwa makosa ya kutoelewana kutokana na lugha wanayotumia.

Tukaiga utamaduni tunaodhani ni bora kuliko wetu. Tunaona madhara ya vijana kuwa wavivu katika kufanya kazi, tunawaona vijana wa kiume wakijiingiza katika ndoa za jinsia moja. Ni utamaduni wa kuiga na faida zake, ni matokeo ya utandawazi na nadi za kwenda na wakati. Yapo mengi katika utamaduni ambayo yanakinzana na utamaduni wetu wa awali.

Tukaiga siasa inayosemwa ya kidemokrasia, watu kupingana kwa hoja na siyo vioja, siasa za wenyewe waliotangulia kiuchumi na ambao wanatutawala kwa ukoloni mamboleo, tunaona siasa yao ni bora kwa maana ya kuwa haki katika Taifa maskini kama letu, tumegeuza jukwaa la siasa kuwa sehemu ya kibarua, leo tunataka haki ambazo kwazo tuliowarithi hawathubutu kuzifanya. Haya ndiyo maendeleo ya kasumba ya kuiga kila kitu hata kama ni cha kijinga.

Tumeiga michezo yao tumeacha yetu, tumeona ya kwao ni bora kuliko yetu bila kuzingatia mazingira ya kwao na kwetu. Huu ndiyo utumwa ambao nauona unavyotukuka katika kizazi hiki cha kwenda na wakati. Tumeiga mambo ya haraka ya kimaendeleo kutokana na ukweli wa kutoamua kuwa wawajibikaji katika jamii inayotutegemea, vijana wetu wanajiajiri katika mitandao wanasahau umuhimu wa shamba, hawalimi tena, hawafundishi tena kilimo cha kisasa.

Tumeiga teknolojia mpya kwao na kuileta kwetu kwa kuunganisha na dhana ya maendeleo tuliyonayo, tumekuwa wajuaji majuha kwenye mambo ya teknolojia na maendeleo, umegeuka kuwa mwiba wa mafanikio ya vijana wa leo, tunatembea na simu na tunataka kila kitu kifanywe na wengine lakini siyo sisi.

Kila kitu tunaiga ili kwenda na dhana inayoitwa ‘kwenda na wakati’ huku tukisahau maendeleo yetu yalipo, lakini pia tunasahau namna ya uwajibikaji wetu katika kazi. Leo hatuzalishi tena, leo tunaagiza hatutumii nguvu kazi yetu katika kutengeneza na kufanya kazi.

Ukienda madukani hatuna tena mali yetu ya kuzalisha ndani, tuna mali ya kuagiza kutoka kwa wenzetu na tukiamini ni bora na yenye kukidhi mahitaji kuliko ambayo tungezalisha sisi wenyewe, hatuna tena kitu cha kujivunia kuwa chetu, hatuna chakula, mavazi, vinywaji, vitendea kazi, dawa na kadhalika.

Haya ndiyo maendeleo ninayoyaona sasa kwa maana ya kupoteza urithi wetu wa asili, kupoteza utamaduni wetu, mali na kizazi cha kichotara. Ni maendeleo ya kurithi na kutukuza mataifa mengine ya Ulaya na kusahau hazina tuliyokuwa nayo. Ni maendeleo ya kukataa asili yetu na kuikubali ya wengine. Tuache ukasumba wa kijinga wa kuiga kila kitu cha ajabu.

Sasa nashauri turudie azimio la kujitegemea, kujitegemea kwa mali zetu na bidhaa zetu, tujitegemee kwa akili zetu na nguvu zetu, tujitegemee kwa utaifa wetu na utamaduni wetu. Hayo maendeleo ya kuazima tuyatumie kujikwamua pale tunaposhindwa na hili limewezekana katika mataifa mengi duniani, na ndiyo maana leo wapo mbali kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni kwa kujitegemea wao wenyewe kama taifa.

 

Wasalaamu 

Mzee Zuzu

Kipatimo. 

By Jamhuri