Mheshimiwa Waziri, naomba nikushike sikio, labda kuna kitu kinaweza kukukumbusha juu ya ugonjwa huu wa mafua makali ambayo sasa yametuletea tafrani kubwa nchini na kusababisha mdororo kwa baadhi ya sekta.

Elimu ni mojawapo ya sekta ambazo zimeathirika sana, si rahisi kujua sasa hivi, lakini siku zijazo tutaanza kuugulia maumivu ya malipo kwa kipindi ambacho tulipoteza hapa katikati kuwapumzisha watoto wasiendelee na masomo.

Yapo mengi yanayozungumzwa juu ya ugonjwa huu hatari wa corona, mengi ya hayo mazungumzo yamekuzwa sana kiasi cha kufanya hata baadhi ya familia kuingia katika mtego wa kuishi maisha ya kubahatisha, hii ndiyo Tanzania ambayo kila mtu ni mwanasiasa na kila mtu ni mwandishi. Ninashukuru siasa ulikataza lakini uandishi watu wanaendelea nao bila kujali kwamba maandiko yao yana athari kiasi gani katika jamii.

Wiki jana nimeandika waraka wangu na kuwausia wanangu kuwa usiku wa deni haukawii kucha, nikasema kuingojea corona ya mbali tutashitukia ikiwa mlangoni, inahitaji kuonana na sisi, na kweli usiku ule haujacha tayari kuna ugeni wa watu wenye maradhi ya corona wakiwa nchini na tumeanza hekaheka ya asiye na mwana kueleka jiwe. Ni kitimutimu

kweli huku kijijini mpaka tunakosea hata maagizo ya wataalamu tunajikuta tumefanya sivyo.

Siku mbili baada ya mgonjwa wa kwanza kupatikana wewe waziri mwenye dhamana ulionekana katika vituo vya habari ukitutaka tutulie, kwani hatua stahiki za awali kwa mgonjwa huyo zinachukuliwa ili kuweza kudhibiti maambukizi, lakini kubwa zaidi ulitutaka tutulie tusiwe na wasiwasi na tuchukue hatua stahiki za usafi na kuepuka misongamano isiyo ya lazima, ulitupa ushauri nasaha na tukaridhika kwa taarifa ile.

Siku ziliendelea na taarifa ziliendelea kutoka katika vyanzo mbalimbali, matangazo yalikuwa mengi kiasi cha kujiona kama vile wewe ndiye mgonjwa hasa wa corona, habari ya mjini ikawa corona, huku tukirejelea habari za Ulaya na vifo vinavyoendelea. Ninajuta sana na ninajiona mwenye upweke mkubwa kipindi hiki ambacho sina mavazi ya kujikinga na sina hizo dawa za kuweka mlangoni kwangu kama tunguri ya kuzuia watu wenye corona kutoniambukiza, bado sijaijua vizuri corona hii yenye vituko kuliko maradhi mengine.

Mwaka jana mwishoni, wengine tulisikia kuna corona huko China, tukatajiwa dalili zake na jinsi unavyoua, wakati tukisikia huko China, hapa nchini kulikuwa na watu wanaugua kitu kama hicho kabisa na walilalamika kwa kutoelezwa ni nini hasa ambacho kinaendelea, hatimaye wizara ikatoa waraka wake siku tano kabla ya Krisimasi kwamba ile hali ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa tu na watu wanywe maji mengi, dawa za kutuliza homa na kupumzika sana na hali hiyo itakwisha kwa wastani wa siku tatu mpaka 14.

Kipindi chote hicho tulikuwa tukipokea wageni mbalimbali kutoka mataifa mengi, sina hakika kama tulikuwa tukiwakagua japo tayari taarifa za corona zilikuwepo huko China, sina hakika kama tulichukua tahadhari kubwa kabla ya ujio wa huyu mgeni corona kama ambavyo sasa tunafanya.

Ile tahadhari ya wizara ni kama inaniambia kitu kwamba kulikuwa na dalili zote za watu kuugua kitu kinachofanana na hiyo hatari, na ni kweli kwamba dalili na maumivu yake ni kama yanataka kufanana, na ni kweli kwamba tahadhari zake ni kama zilezile za ule ugonjwa ambao tulielezwa unatokana na mabadiliko ya hali ya hewa na ugonjwa uliitwa ‘Influenza’.

Najiuliza, Mheshimiwa Waziri, hivi dalili zile za wataalamu wetu kwamba ni homa kali, mwili kuchoka, kichwa kuuma, mafua, kikohozi, kupata mafindofindo, kupiga chafya,  kuharisha na kutapika ni tofauti na hizi za corona? Kama sivyo tulikuwa wapi kuchukua hatua mapema kukabiliana na maradhi haya? Naogopa kusema, labda kuna dili mahali ambayo Wachina waliificha ikawa tofauti na hii homa yetu.

Taharuki iliyopo mtaani ni kubwa mno, sasa tunaelekea kununua ugonjwa mpya wa bakteria kwa watu kuvaa maski moja wiki nzima wakiamini ndiyo kinga ya corona, tujiandae kuzalisha ugonjwa mpya baada ya ujio wa corona, naamini kuna ombwe kubwa la taarifa kwa umma juu ya mambo mengi yahusuyo afya na hili ni mfano tu.

Nachelea kusema influenza ile ya wizara ni tofauti kabisa na corona yetu mpya.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

395 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!