Wanangu, naanza kwa kusema nawapenda sana na siku zote nitakuwa pamoja nanyi katika maombi, ili mpate kuwa na siku nyingi za kuishi kama mimi nilivyobarikiwa  kutimiza miongo mingi kidogo. Nimefika miongo hiyo kutokana na kuwaheshimu wazazi wangu ambao ni miungu wangu hapa duniani.

Wanangu, kuna wakati najisikia vibaya ninapoona mnakabiliwa na viashiria vingi vya vifo na hasa mkiwa bado katika umri mchanga kabisa wa miaka arobaini au hamsini tu.

Wanangu, leo nianze kuwaeleza kuwa simba mzee siku zote anaishi mtoni, karibu kabisa na mahala ambapo swala, paa, pundamilia na wanyama wengine wanakunywa maji. Lengo lake ni kudidimiza kila mnyama anayejipendekeza kuja mtoni. Nimetoa huu mfano lakini ukweli ni kwamba mimi ni simba mzee.


Wiki jana niliwasimulia na kuwakanya juu ya aina ya michezo ambayo watoto wenu wanacheza na athari zake katika maisha yao, labda sikuweza kusema wazi kwamba mwisho wa yote hayo ni kuwa na mitoto mivivu kufanya kazi na kuishia kuwa majizi au majambazi; na ikitokea hayana nguvu kama ni ya kiume basi huwa mishoga na kama ni ya kike huwa michangudoa.


Ukishindwa yote hayo, unaweza kubarikiwa kuwa na mdomo wa cherehani na kutengeneza mazingira ya kuwa mwizi wa mdomo. Unaweza kuwa tapeli na siku ukishikwa na wasamaria wema watakuchapa na kukuacha uende ukajifunze tabia njema. Lakini siku ukishikwa na Mzee Zuzu kamwe hakuachi uende ukajifunze tabia njema – kuna mawili, nikiwa na huruma sana basi nitakutoa meno ya mbele ili ushindwe kupanga sentesi za kitapeli vizuri, lakini kama ni siku mbaya basi utatangulia ‘guest’ ya bure ya Serikali pale Muhimbili au Temeke, Mwananyamala, KCMC na nyingine nyingi zilizoko katika kila wilaya na mimi nitajipeleka mwenyewe jela.


Zamani nilikuwa mhuni tena bitozi kwelikweli. Anayenijua atakwambia kuwa Mzee Zuzu ndiye Mtanzania wa kwanza kumchapa makonde Mchina pale Msamvu, Morogoro mchana kweupe wakati huo wa akina Bruce Lee na wenzake wa kwenye filamu. Wakati huo nilikuwa naitwa mshoka, yaani mhuni kuliko wahuni wa kizazi hiki cha dotcom. Nashindwa kufananisha uhuni wa mshoka na mhuni wa leo, sijui nimwiteje mhuni wa leo ili aweze kufanana na Mshoka mimi wa enzi zangu.


Nilikuwa naweza kupanda basi kwenda Morogoro bila nauli, nikiulizwa nauli nawachapa makofi kuanzia kondakta, dereva na abiria yeyote atakayeleta kimbelembele cha kuhoji sababu ya kupigwa kwa wenzao. Mimi ndiyo mshoka wa enzi hizo ambaye sijachoka hivyo bado ni mhuni mzee.


Wapo baadhi wanaotaka kuingia kwenye anga zangu, lakini kwa bahati nzuri wanatokea kwenye tundu la sindano na wale wachache wanaokosea kidogo basi naamini baadhi yao ukiwaambia watamke neno maji utamsikia akisema mayi, au neno thubutu utamsikia akisema suwutu. Ukikutana na mtu mwenye matamshi hayo jua kuwa aliingia kwenye mtego wangu mzee wa Kipatimo.


Uhuni wetu ulikuwa wa kutumia nguvu zaidi na si wa maneno. Uhuni wa maneno unatokana na uvivu ambao kila siku Mzee Zuzu nalalamika kuwa ni bomu tishio la kizazi hiki. Nahofia hili bomu likiendelea, hatimaye sijui itakuwaje, labda tutaanzisha taifa jipya la kisanii na kufa na njaa.


Wanangu, nimeamua leo niwaandikie kwa nia ya kuwajuza wale ambao hamjakutana na wahuni wa dotcom, ambao kwa akili yao nyepesi wanadhani wataendelea kuishi maisha haya ya kubahatisha, kutapeli bila kubuni njia madhubuti ya kukabiliana na njaa halisi iliyoko mbele yao.

 

Utapeli una kikomo, kama wanashindwa kujiandaa vyema sasa na nguvu ambazo wamejaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa nazo. Kama mimi msuba wa zamani ningeulizwa leo, basi ningesema nguvu zangu nazielekeza katika kilimo ili siku moja nisiwe tapeli wa barabarani, nikae mtoni kungoja anayeingia katika anga zangu.


Siku za hivi karibuni kumeingia utapeli mwingi wa kidotcom na wanaoibiwa ni dotcom zaidi kwa sababu wanatumia mitandao mnayodhani ni maendeleo kumbe ni umaskini unaowanyemelea bila kujua. Watu wanatumia simu kuibiana fedha bila kujali athari ya kukamatwa na matapeli wenzao wastaafu.

 

Upo ujanja au utapeli watu wanaojifanya wanatafuta madini ya aina fulani na wanatoa namba za simu ili wenye kutaka fedha za haraka waingie kwenye mtego wao, wanawapata kwa urahisi lakini bahati mbaya wote wanaopatikana ni walewale wa dotcom wanaoishia kuwalaumu polisi kwamba hawafanyi kazi yao. Najiuliza, mbona inapotokea mkapata hamuwashirikishi TRA na polisi?


Wapo wajanja na matapeli wa kijinga wanaochukua namba ya mtu wanayemfahamu na kutaka kumhusisha na biashara ya dawa za kilimo ama mifugo. Hawa wamefika mbali na wana mtaalamu kabisa kazee ka Kijermani ambako huunganisha Kiingereza cha Kijermani hadi anayetapeliwa huingia kwenye mtego na hatimaye kuchukua amana yote ya aliyetapeliwa.

 

Nendeni vituo vya polisi mkaone vidhibiti vya kitapeli vilivyojaa kwa kigezo cha maisha ya haraka haraka, na wenye haraka hiyo ni walewale wa dotcom na madhara yake kila aliyetapeliwa naye hutafuta  wa kumtapeli –  hapo ndipo ajira inapopatikana. Hivi mmewahi kujiuliza hatimaye nani atalima ili tule?


Wanangu, nasema hivi kwa sababu kila kitu kina mwisho wake, sisi tulifanya uhuni lakini tukafika mwisho na kuanza kujilaumu kwanini hatukutumia muda huo kupanda miti ambayo labda tungekuwa tumevuna na tunakula maisha mazuri kivulini. Tulipoteza muda mwingi kujifunza mambo ya “oliva na ngai” huko Zaire wakati huo, lakini tukaishia kuonesha mazingaombwe hayo katika shule za msingi hadi yalipopigwa marufuku.


Wapo wahuni wengine ninaodiriki kusema muda si mrefu wataanza kushindwa kutamka vizuri maneno na hasa kama watakutana na akina Mzee Zuzu, ambao kwao kutoa kichapo cha mbwa mwizi ni jambo la kwaida.

 

Wanajifanya wapo katika vikao na wanaomba watumiwe fedha kwa ndugu zao ili wakitoka katika semina na vikao warejeshe! Bahati mbaya sana hutumia majina ya watu wenye heshima katika jamii kwa wao kujifanya ndiyo wenyewe, na wanaotumiwa majina yao hawajui kuwa wanabaki na madeni katika jamii inayowazunguka! Hawa nasema ole wao! Siku zao si tu kwamba zinahesabika, lakini pia yawezekana ikawa leo ndiyo mwisho wao! Lakini swali langu utawadanganya wangapi hadi utakapofikia umri wangu na usiwe umegundulika?


Wanangu, njia pekee si karata tatu kwamba cheusi ndicho cha hela kekundu na kekundu utaliwa, bali ni kujua wewe ni nani katika jamii na unapaswa kufanya nini kwa wakati huu. Ni bora apandaye mti mmoja leo na akalala baada ya miaka michache atavuna, lakini wewe mavuno yako yanaweza kuwa siku yoyote itakapotimia arobaini yako, utajuta kuzaliwa tapeli.


Wanangu, haya ni mazao yetu baada ya kukataa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kusutana katika uvivu wa kazi na baada ya kubariki biashara za udalali na kuzipa vibali halali kwa majitu yenye afya njema za kukata ekari za mashamba. Haya ndiyo matokeo ya sayansi na teknolojia ya kuamini siku moja unataka kuwa kama Bill Gates bila kutoa jasho, maisha ya kutaka kuwa na fedha bila kujua zinatoka wapi na umewaumiza watu wangapi?


Wanangu, haya ndiyo maisha tunayotegemea kizazi kijacho kiishi hivyo. Kwamba nchi nzima inakuwa ya matapeli na tutaendelea kutapeliana hadi itakapotungwa sheria ya kulinda matapeli kama hatutaamua kuchukua sheria za mkononi za Mzee Zuzu kulinda heshima ya taifa letu si lenu.


Wanangu, nitawajuza mengine lakini nasema mimi ni simba mzee, mtasikia siku moja nimekula swala na mtawaona wanaoshindwa kutumia meno ya mbele kutamka. Siku njema.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

0784-232768

1276 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!