Wakati hekaheka za Uchaguzi Mkuu wa 2015 zimeisha hapa nchini, kwa washindi kupatikana ikiwa ni pamoja na mshindi wa kiti cha urais na chama tawala, nimegundua kwamba kumbe bado tunayo mengi ya kujifunza katika nyanja ya siasa.

Nimeliona hilo baada ya kuulinganisha Uchaguzi huu Mkuu wa Tanzania kuwa haulingani na chaguzi nyingine katika baadhi ya nchi, tena zilizo barani Afrika.

Tofauti na tunavyopendelea kujionesha mbele ya jumuiya ya kimataifa, kwamba Tanzania ni nchi komavu kisiasa, nchi ya amani na utulivu; ukweli ni kwamba bado tunayo mengi ya kujifunza kuhusu mambo hayo na safari ndefu ya kuifikia hali hiyo tunayotaka kuonesha kuwa tunayo kwa sasa.

Kama siyo kwa makusudi, basi inawezekana uelewa mdogo tulio nao katika mambo hayo kwa kiasi kikubwa ndiyo unaotufanya tujione hivyo.

Wahaya wanao usemi wa kwamba “omwana atalya mumaju ati mae amanya kuchumba kukila abantu bona”, ukiwa na maana ya kwamba mtoto asiyezoea kula kwingine mbali na nyumbani kwao husema kwamba mama yake ndiye anayejua kupika vizuri kuliko watu wote! Ni sababu haelewi kwingine kunapikwaje.

Siku ya uchaguzi, Jumapili iliyopita ya Oktoba 25, 2015, niliandika makala nikisema kwamba uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni nafasi pekee ya kuidhihirishia dunia kuwa amani tunayoiimba nchini kwetu ni ya kweli, nikaongeza kuwa amani ni tunda la haki, pasipo na haki amani hakuna. Sababu penye haki hakuna malalamiko wala vinyongo.

Inapotokea kwamba hali itakuwa hivyo, kwa maana ya kila mmoja kuridhika na alichokipata, hapawezi pakawapo na tishio la kwamba amani itavurugika na hivyo kulazimika kuweka mikakati ya kuilinda amani; kitu pekee cha kuilinda amani ni kutendeana haki, basi.

Hivyo, zinapotayarishwa zana kalikali kwa kisingizio cha kuilinda amani inapaswa ieleweke kwamba hapo haki hakuna na amani ni lazima iwe mashakani.

Siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu, nilimuona Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete, akilikabidhi Jeshi la Polisi zana mpya na kalikali za kisasa kama sehemu ya kuliimarishia uwezo wake wa utendaji kazi. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, akasema kwamba zana hizo zisihusishwe na suala la Uchaguz Mkuu.

Lakini tangu lini majambazi, kwa mfano, ambayo ni jukumu la polisi kulinda uovu wao usitendeke dhidi ya wananchi yakashughulikiwa kwa maji ya kuwasha na mabomu ya machozi? Bila shaka hizo ni zana zinazotumiwa na polisi dhidi ya wananchi wanaodaiwa wana amani pale wanapokuwa wanalalamikia haki kutotendeka. 

Sababu kama haki inatendeka hakuna awezaye kulalamika kiasi cha kulilazimu Jeshi la Polisi kutumia nguvu ya ziada kwa kutumia nyenzo hizo, maji ya kuwasha, mabomu ya machozi na zana nyingine nzitonzito. Kwa ufupi naweza kusema kwamba mara zote zana hizo zinatumika dhidi ya wapenda haki.

Jambo hilo linaweza kutafsiriwa kwamba zana za aina hiyo, ambazo tena zinanunuliwa kwa kodi za wananchi, mara zote zinatumika kuipoteza amani ikichukuliwa kwamba amani ni tunda la haki.

Jingine ni kwamba wakati Uchaguzi Mkuu ukikabiliwa na changamoto lukuki zinazotokana na jiografia ya nchi yetu pamoja na ukata ilio nao, badala ya kukitumia kidogo tulicho nacho kujaribu kuzipunguza changamoto hizo ili kufanikisha lengo letu kuu, uchaguzi nchi unatumia kiasi kikubwa cha pesa kuagiza zana za kuwafanya wananchi watulie hata pale wanapoona haki yao inapindishwa. Tuseme utulivu wa aina hiyo ni wa amani au ni wa hofu inayojengwa na zana hizo za kutisha?

Na kama hali iko hivyo, nani anayehatarisha amani iliyopo nchini kati anayetaka kupora haki na anayedai haki?

Tofauti na sasa, chaguzi za miaka ya nyuma kabla ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa,  tuseme mpaka Uchaguzi Mkuu wa 1990, mambo yalikuwa yakienda kwa raha mustarehe. Ndiyo, polisi walikuwapo kwenye sehemu za kufanyia uchaguzi lakini wakiwa na kazi ya kuwaelekeza wapiga kura wajipangeje na mambo mengine kama hayo bila ya kuwa na silaha za aina yoyote. 

Wakati huo hali ilikuwa ni ya amani kwa maana halisi. Siyo kama sasa ambapo, mbali na polisi kuwa na silaha za kila aina, pia wanavaa mavazi ya kutisha kana kwamba wanaenda kwenye vita iliyoko sayari nyingine tofauti na duniani! Je, hiyo ndiyo amani kwa mtindo wa leo?

Nikumbushe kwamba kuna kashfa kubwa ya kisiasa iliyowahi kutokea nchini Marekani “The most notorious political scandle”, Kashfa ya Watergate. Kashfa hiyo ya mwaka 1972 ilimlazimisha rais wa 37 wa nchi hiyo, Richard Milhous Nixon, kujiuzulu mwaka 1974.

Kashfa hiyo imekuwa ikitajwa mara kwa mara hata hapa nchini kwetu kama alama mbaya ya ukiukwaji wa maadili katika mfumo mzima wa kisiasa. Ila nahisi walio wengi hapa nchini kwetu hawaelewi ilikuwa ni kashfa ya aina gani. Maana niliwahi kuona baadhi ya waandishi hapa nchini wakiifananisha na kashfa ya uhujumu uchumi iliyotokea Loliondo kiasi cha kuandika eti hiyo nayo ni Loliondogate!

Kwa ufupi ni kwamba Watergate ni jengo yalimokuwa makao makuu ya chama cha siasa cha Democratic, moja ya vyama viwili vikuu vya siasa nchini Marekani. Wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani wa mwaka 1972 wapambe wa chama tawala cha Republican, waliokuwa kwenye mikakati ya ushindi wa chama chao, walifanya mbinu za kuingia kwenye ofisi za chama hicho cha upinzani kwa lengo la kuiba nyaraka za siri za upande huo wa pili ambazo walizitumia kwenye harakati za ushindi wa chama chao.

Pamoja na hilo, pia waliweza kupata majina ya baadhi ya makada wa Democratic ambao walinyanyaswa sana na vyombo vya dola vya nchi hiyo vya FBI na CIA, kwa makosa ya kubambikiziwa kwa faida ya chama tawala. Lakini, hata hivyo, waliingia katika ofisi hizo kwa njia ya siri sana, hawakuingia kimabavu.

Baada ya uchunguzi huru nchini Marekani kuonesha kuwa suala hilo lilihusiana na kampeni za Rais Richard Nixon, ndipo ilipobidi awajibike mwaka 1974 akiwa mwanzoni mwa kipindi chake cha pili cha urais.

Tukio hilo halitofautiani sana na tukio la polisi hapa nchini kwetu kuingia kwenye sehemu ya Chadema na kuwakamata wataalamu wake wa mawasiliano ya kompyuta, waliokuwa wakikusanya takwimu za uchaguzi kwa ajili ya chama chao pamoja na vifaa vilivyokuwa vikitumika kwenye shughuli hiyo. Tofauti pekee inayojionesha ni kwamba wale wa Watergate walitumia ujanja wa kuingia kwenye ofisi za upinzani wakati hapa wametumia mabavu, lakini lengo likiwa ni moja.

Siendi mbali kwenye suala hilo sababu tayari liko mahakamani. Ila kutokana na kufanana sana kwa matukio hayo mawili ndiyo maana nauliza kwamba Watergate imehamia Tanzania?

 

[email protected]

0784 989 512

By Jamhuri