Timu ya Yanga imeendelea kugawa dozi kwenye Kombe la FA, baada ya kufuzu kuingia katika hatua ya nusu fainali, baada ya kuwatupa nje ya michuano hiyo timu ya Alliance kwa jumla ya penalti 4-3 katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1.

Katika hatua hiyo ya robo fainali, mchezo huo wa Alliance dhidi ya Yanga ndio wa kwanza kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, baada ya michezo mingine kumalizika katika dakika 90.

Mara baada ya timu ya Alliance kusawazisha goli katika dakika ya 62, walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo licha ya Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kufanya mabadiliko kadhaa kwa kuwaingiza viungo kama Thabani Kamusoko.

Mara baada ya mpira kumalizika na ile penalti ya ufunguzi ambayo Kelvin Yondani alikosa baada ya kugonga mwamba wa goli, mashabiki wa Yanga walibaki wakiduwaa, wakihisi wameyaaga mashindano, lakini haikuwa hivyo. Uhodari wa golikipa wao, Klaus Kindoki, kucheza penalti mbili kukarejesha matumaini kwa Wanajangwani hao kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.

Yanga imepambana kwelikweli kwenye Kombe hili la FA, kwani kabla ya kuingia robo fainali ilichuana na timu ya Namungo kutoka mkoani Lindi, katika hatua ya 16 bora na ikafanikiwa kuwabwaga nje ya mashindano baada ya kuibuka na ushindi wa goli 1-0 katika Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi. Vilevile iliwatoa nje ya michuano hiyo timu ya Biashara United kwa jumla ya mikwaju ya penalti 5-4 katika dimba la Uwanja wa Taifa.

Kutokana na ushindi huo, Yanga itavaana na timu ya Lipuli ya Iringa katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika dimba la Samora, mkoani Iringa, mtanange unaotazamiwa kuwa wa kukata na shoka kutokana na timu zote kulipigia hesabu kali Kombe hilo la FA ili hatimaye waweze kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga imeingia nusu fainali ya Kombe la FA licha ya kuwakosa nyota wao kadhaa katika mchezo huo kwa sababu mbalimbali. Nyota hao ni pamoja na Gadiel Michael, Ibrahim Ajibu, Ramadhani Kabwili na Abdallah Shaibu.

Sasa timu ya Lipuli itamenyana na Yanga baada ya kuwatupa nje ya mashindano ya FA Singida United kwa kuichapa katika Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.

Vilevile timu ya Azam imefanikiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali baada ya kuwatupa nje ya mashindano Kagera Sugar katika dimba la Kaitaba, mkoani Kagera, nao watachuana na timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) katika dimba la Uwanja wa Uhuru.

Haikuwa rahisi timu ya Yanga kuingia katika hatua ya nusu fainali na baada ya droo kuwakutanisha dhidi ya Lipuli, timu ya Yanga ina kibarua kigumu kuhakikisha wanaingia katika hatua ya fainali.

Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi timu kutoka kusini mwa Tanzania zimekuwa zikiipa wakati mgumu Yanga wanapocheza katika viwanja vyao vya nyumbani. Si Lipuli tu, bali hata timu ya Majimaji kutoka Songea kabla haijashuka daraja pamoja na Ndanda kutoka Mtwara zimekuwa zikitoa upinzani mkali dhidi ya Yanga zinapocheza nyumbani. Je, Yanga itaweza kutetema mbele ya Lipuli? Muda utazungumza.

By Jamhuri