Ikiwakilishwa na timu nne za Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club, Dar es Salaam Young Africans (Yanga), Azam FC zote za jijini na Mafunzo kutoka Zenji katika hatua za awali za michuano ya Kombe la Kagame, Tanzania ilipata fedheha kubwa katika mechi zilizochezwa siku ya kwanza na ya pili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ilifungua dimba kwa kuchapwa mabao 2- 0 na Atletico ya Burundi na kesho yake, Simba ikapokea kichapo cha idadi hiyo ya mabao kutoka URA ya Uganda. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kabla ya timu hizo kushinda kila moja zilipocheza mara ya pili.

 

Yanga iliichakaza Wau al Salaam ya Sudan Kusini kwa mabao 7-1 huku Simba ikiishushia mabao 3- 0 Ports ya Djibouti, timu mbili zilizokuwa dhaifu kuliko zote zilizoshiriki hatua ya makundi kabla ya kuanza kwa robo fainali jana Jumatatu. Sitazungumzia chochote mechi zote zilizofuatia kwa timu hizo kucheza wala za Mafunzo ama Azam FC.

 

Pamoja na Yanga kubadilika katika mechi ya tatu ilipocheza dhidi ya APR, Ijumaa iliyopita na kushinda mabao 2-0 na kuingia robo fainali, ukweli kwamba ilianza vibaya michuano hiyo inayomalizika Jumamosi wiki hii, unabaki palepale na vilevile. Ilianza utadhani timu iliyokuwa imekusanywa ghafla, jambo lililorudiwa na Simba kesho yake tu.

 

Hata ilipokuja kuikung’uta Wau al Salaam haikustahili kupata ushindi ule mwembamba, tena ikicheza kwenye uwanja wa nyumbani na mbele ya mashabiki wake wa siku zote. Ilitakiwa kupata ushindi mkubwa kupindukia lakini ikashindwa.

 

Ilikuwa ni sawa na Barcelona ya Hispania kucheza na AFC Leopards au Gor Mahia kutoka Kenya kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Nou Camp, kisha ipate ushindi kiduchu kiasi hicho. Simba nayo ilipoichapa Ports mabao 3-0 haikustahili kupongezwa. Ilikuwa ni kama Chelsea ya England kucheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Stamford Bridge jijini London halafu ikaambulia ushindi huo!

 

Sudan Kusini iliyopata Uhuru wake Julai 9, mwaka jana walipojitenga na Sudan Kaskazini, si lolote si chochote kisoka. Bado ni kama mtoto wa miaka mitano apigane na kijana mwenye umri wa miaka 20 na hivyo lazima apigwe Knock Out (KO) hata iweje, tena dakika ya kwanza tu. Yanga na Simba zilipocheza na timu hizo nilitarajia zipate idadi kubwa ya mabao kuliko 7-1 au 3-0. Zote zilitakiwa zipate angalau ushindi wa mabao 10-0 lakini zikashindwa.

 

Fikiria kwa mfano mshambuliaji Felix Sunzu wa Simba alivyoshindwa kupata bao lolote kwa shuti la kawaida. Tazama alivyocheza kama mshambuliaji wa timu ya daraja la sita aliyeletwa ghafla kucheza ndani ya ligi kuu, tena kwa michuano mikubwa kiasi hicho na kutaharuki. Kama asingepiga penalti katika dakika ya 64 kutokana na beki Jean Paul kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari hakika asingefunga.

 

Sunzu aliyewahi kuichezea timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo) na kutemwa kwa kushuka kiwango chake, aliinyima pia timu yake hadi mabao ya wazi. Kila anapopata nafasi nzuri ya kufunga alikuwa akipata kigugumizi miguuni mwake ama vinginevyo na kushindwa.

 

Hata kocha wake, Cirkovic Milovan ameliona waziwazi pengo lililoachwa na mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Emmanuel Okwi anayefanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa huko Italia. Amesema kutokuwapo kwake ni pigo na hana mshambuliaji yeyote anayeweza kuibeba Simba inapokuwa uwanjani.

 

Katika viwango vilivyotolewa na Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) mwezi huu, Tanzania ilishika nafasi ya 39 kwa ubora wa mchezo huo barani Afrika, halafu Djibouti ikiwa ni ya 52 na Sudan Kusini haijaanza hata kuhesabiwa.

 

Katika hali hiyo, hatua ya Simba kushinda kwa mabao 3-0 tu dhidi ya Ports haina maana. Waliofika Djibouti wanaelewa kuwa hakuna hata uwanja wa kandanda unaoweza ukapewa heshima hiyo. Kwa mfano timu hiyo ingecheza na klabu bingwa ya soka kutoka nchi za Cameroun, Nigeria, Ivory Coast, Ghana, Morocco au Tunisia ingechapwa hadi mabao 20 bila kujali mechi hiyo imechezwa wapi.

 

Mbali ya Sunzu kutokuwa lolote dimbani kwa siku hiyo, hata mshambuliaji mpya wa Simba, Abdallah Juma aliyesajiliwa na timu hiyo msimu huu kutoka JKT Ruvu naye hakuonyesha makali yaliyotarajiwa. Alicheza kama amelazimishwa na kocha wake, hivyo naye akaamua kucheza ilimradi tu yupo uwanjani huku akili yake yote ikiwa nje. Goli alilolikosa akiwa amebaki na nyavu, linashusha heshima hata ya mabao mawili aliyopiga.

 

Mbali na mabingwa hao wa kandanda wa Tanzania Bara, Yanga pia iliacha maswali mengi ilipoifunga Wau al Salaam kwa mabao 7-1 tu. Ikiwa tayari imefunga mabao 6-0 hadi kinamalizika kipindi cha kwanza, timu hiyo ambayo sasa inanolewa na Uncle Tom kutoka Ubelgiji, ilishindwa kufurukuta katika kipindi cha pili.

 

Hata washambuliaji wake mahiri akiwamo Saidi Bahanuzi aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, Khamis Kiiza na hata viungo tegemeo kama Nizar Khalfani, Haruna Niyonzima na Athuman Idd (Chuji) waliotarajiwa kufanya mambo makubwa, walionekana kulewa sifa waliporudi mara ya pili dimbani.

 

Ikiwa tayari iko mbele kwa mabao 6-0 hadi mapumziko ambayo yalifungwa mfululizo, Yanga ilidhaniwa kuwa ingevunja rekodi iliyowekwa na Pamba ya Mwanza ilipoichapa timu ya Anse Balou ya Mauritius mabao 12-0. Ilikuwa katika michuano ya Kombe la Washindi barani Afrika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini humo.

 

Badala ya kufanya hivyo kwa Yanga au hata kuifunga Wau al Salaam kwa mabao 15-0, ushindi uliokuwa unawezekana, ghafla upepo uligeuka katika kipindi cha pili kwa timu hiyo kucheza soka la ovyo. Wachezaji wake ambao kwa dakika 45 za kwanza walionyesha nia na uwezo wa kutengeneza rekodi isiyovunjwa sasa wala baadaye, waligeuka na kuwa vimeo waliporudi tena dimbani.

 

Kasi na uchu wa kuzifumania nyavu uliokuwapo mwanzo ukakosekana. Hata mshambuliaji tegemeo kuliko wote wa timu hiyo hivi sasa, Saidi Bahanuzi naye alishindwa kuwa lolote wala chochote. Badala ya kutafuta mabao zaidi na hasa baada ya kupata mawaidha mapya kutoka kwa kocha wao, wachezaji wa Yanga walianza kubutua mipira katika hali ambayo ingedhaniwa kwamba wanajifunza kandanda.

 

Waliipa nafasi Wau al Salaam ya kuanza kuonekana uwanjani ikilinganishwa na kipindi cha kwanza ilipokuwa ikipelekwa marikiti mara kwa mara. Kama mchezo huo ungekuwa unachezwa kwa dakika 120 na si 90, hakika mabingwa hao wa Sudan Kusini wangeweza kusawazisha mabao yote waliyofungwa na kutoka sare na hata kushinda mechi hiyo.

 

Wakati Yanga ikiongeza bao katika dakika ya 75 lililofungwa na Nizar Khalfan, wachezaji takriban wote wa timu hiyo walishachoka kuendelea na mchezo na kubaki wakirukaruka tu. Hapo ndipo mshambuliaji tegemeo wa Wau al Salaam, Khamis Deshama alipotikisa nyavu katika dakika ya 90 na kufanya matokeo yabadilike na kuwa mabao 7-1.

 

Je, kiwango kilichoonyeshwa kinapaswa kuvumiliwa? Tunasema hapana. Simba na Yanga kama ziko ‘serious’ lazima zibadili kiwango hiki kibovu. Hakikubaliki.

1033 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!