Wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club ya jijini ikifanya vizuri kwa kujikusanyia pointi nyingi mwanzoni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mahasimu wao wakubwa zaidi, Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake mitaa ya Jangwani na Twiga, imekuwa ikisuasua na kuzua maswali mengi kutoka kwa mashabiki wake.
Kabla ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Alhamisi iliyopita, Yanga ilifungwa bao 1-0 na wakata miwa wa Kagera Sugar mjini Bukoba, mechi iliyotazamwa kama rahisi zaidi kwake kuliko zote ilizocheza mwanzo.

Simba imekuwa ikionesha dhamira ya dhati ya kutetea ubingwa wake, lakini Yanga inacheza kama haijadhamiria kulirudisha taji hilo ililolipoteza msimu uliopita. Hali hiyo ni kinyume cha matumaini ya mashabiki wake baada ya aliyekuwa mfadhili wake mkubwa, Yussuf Manji, kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Awali, Yanga ilijikuta ikipoteza michezo miwili ikianzia Morogoro ilikofungwa na wababe wa Mtibwa Sugar na kusababisha aliyekuwa kocha wake mkuu, Mbelgiji Tom Saintfeit kufukuzwa na kuletwa raia wa Uholanzi, Enerst Brandts.

Katika mchezo wake dhidi ya Simba zilipotoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga walionekana kuwadhibiti kwa kiasi mahasimu wao hao. Mtanange huo ndiyo chanzo cha mwamuzi Mathew Akrama kusimamishwa kazi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Lakini Yanga ilipofungwa na Kagera Sugar, mashabiki wake walifarijika kidogo, na kama ingefungwa pia na Toto African huenda wangepoteza kabisa matumaini ya timu hiyo msimu huu.


Mashabiki hawajapata jibu la Yanga kufanya vibaya msimu huu wakati ina wanasoka mahiri wakiwamo Saidi Bahanuzi “Balotelli’, Didier Kavumbagu, Nurdin Bakari, Athuman Idd “Chuji’, Khamis Kiiza, Nadir Haroub “Cannavaro’, Haruna Niyonzima “Fabregas’, Frank Domayo, Shamte Ali, makipa Yaw Berko na Ali Mustafa ‘Berthez’.

Hata kocha msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, alishindwa kusema chochote baada ya timu hiyo kuadhiriwa na Kagera Sugar mjini Bukoba.


1013 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!