‘Uongozi ndiyo unaozaa utawala’

 

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne – watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Utandawazi umetuletea wimbo mpya unaosisitizia utawala bora. Wazungu wametupotosha kwa mara yanyingine, wametuaminisha kwamba tunaweza kuwa na utawala bora unaozingatia sheria wakati hicho ni kitu kisichokuwako.

Kwa namna utawala ulivyo hauwezi kuboreshwa hadi watu wakaiona tofauti ya ubora kati ya utawala fulani na utawala mwingine. Kimsingi utawala unaweza kuzidiana katika umakini kwamba utawala mmoja unaweza kuwa makini kuliko utawala mwingine, lakini hauwezi kuwa bora kwa kuwa utawala hauboreshwi.

Kinachoweza kuboreshwa ni uongozi, maana ili nchi ifanikiwe inahitaji kuwa na uongozi bora kwa sababu uongozi bora ndiyo unaoweza kuunda Serikali makini itakayotawala watu kwa umakini. 

Wakoloni hawakutufundisha somo la uongozi bali walitufundisha utawala na uendeshaji yaani ‘management and administration’ kwa sababu mkoloni hakutaka malengo yake yakwame, wala hakutaka kazi zake kwenye ofisi za serikali ziendeshwe kiubabaishaji.

Mwingereza alipounda mamlaka ya BOMA yaani ‘British Overseas Management Authority’ alikusudia uendeshaji wa makoloni yake yote uwe wa uhakika na ufanisi, alitaka mambo yote yafanyike kitaalamu. Kwenye masuala ya utawala, uendeshaji na usimamizi, Mwingereza alifaulu ndiyo maana katika miaka yote 40 aliyotawala hakukabiliwa na maasi kutoka kwa wenyeji (watawaliwa) kama utawala wa mtangulizi wake, Mjerumani, ulivyokabiliwa na maasi (vita ya Majimaji) kati ya mwaka 1905 na 1907. 

Mwingereza alikuwa na mameneja wazuri waliofundishwa menejimenti, alikuwa na waendeshaji mahiri waliofundishwa ‘administration’ lakini meneja, mwendeshaji na mwelekezaji (director) si viongozi ni wataalamu wanaotakiwa kufanya shughuli zao chini ya uongozi bora.

Wakati wakoloni wakituletea magavana wa kututawala na kutufundisha sisi Waafrika masuala ya ‘management and administration’ wao wenyewe kwenye nchi zao waliwafundisha watu wao uongozi kwa ajili ya kuongoza mataifa yao.

Wakati wakoloni wakituzalishia wataalamu wa shughuli za ofsini yaani watawala, waendeshaji, mameneja na wakurugenzi ili mambo ya ofisini kwenye koloni lao yaendeshwe kitaalamu, mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yaligusa maisha yetu tukiwa kama ‘wakoloniwa’ wao kwenye nchi zao waliendelea kuwa na vyuo vya uongozi wakiwafundisha watu wao yote mawili yaani uongozi na utawala. 

Baada ya nchi zetu kupata uhuru ziliendelea kuzalisha watawala yaani ziliendelea kuzalisha mameneja, waendeshaji na wakurugenzi wa kusimamia masuala ya maofisini. 

Nchi zetu tangu mwanzo tulipoanza maisha mapya kama mataifa huru zilikosa uongozi, maana yake halisi ni kwamba nchi huru za Afrika zilikabiliwa na ombwe la uongozi ingawaje zilikuwa na marais walioongoza serikali zilizotawala watu. 

Kukosekana uongozi kulisababisha kukosekana ubunifu kwani uongozi ndiyo unaopaswa kubuni mambo mapya na kuyashusha kwa watawala ili kwa kuwatumia wataalamu ambao ni waendeshaji, mameneja na wakurugenzi waweze kufanikisha kitaalamu hayo yanayobuniwa. 

Katika kitabu cha Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka kwenye somo la kutoka ukoloni hadi uhuru – miaka 50 ya kutangatanga, nimeeleza sababu za kushindwa kwa Azimio la Arusha.

Sababu mojawapo iliyoikwamisha falsafa ya Nyerere hadi ikashindwa ‘tucope’ na uhalisia wa maisha ya siku kwa siku ya Mtanzania ni ukweli kwamba wasomi na wanataaluma walilisusia Azimio la Arusha. Hawakutoa mchango wao wa kisomi wala mchango wa kianazuoni, wala mchango wa kitaalamu. 

Hakuna uhakika kama wanasiasa walioongoza serikali kisiasa ndiyo waliowaengua wasomi na kutotaka kuwashirikisha kwenye shughuli zao za uendeshaji wa dola. Hakuna uhakika kama wasomi, wataalamu na wanazuoni ndio waliojiweka kando na ubabaishaji wa wanasiasa, wakaamua kujiweka mbali wakabaki watazamaji wanaoangalia jinsi wababaishaji walivyoiharibu nchi.

Lakini historia itaufunua ukweli mkosaji ni yupi kati ya wanasiasa na wasomi ama ni makundi yote mawili, kimsingi hakuna lolote linalofanikishwa nje ya utaalamu, Azimio la Arusha lilipokosa mchango wa wataalamu, mengi yaliyobuniwa na uongozi yalipofikishwa kwenye utekelezaji yalikwama. 

Kwa sababu hayakutekelezwa kitaalamu, mazuri yaligeuka kuwa tasa yaani yasiyozaa matunda mazuri, mambo mazuri yalipofanywa vibaya yalitoa matokeo mabaya. Ndipo wengine wakaihukumu siasa ya Ujamaa na Kujitegemea wakaiona ni siasa iliyoshindwa, wengine wakaiona ni siasa mbaya hata kama hawakusema hadharani kwamba Ujamaa hautufai.

Waliolaumu hawakutambua kwamba kukwama kwa mipango mizuri kulisababishwa na kosekana kwa mchango wa utaalamu, kama wataalamu wangetoa mchango wao wa kitaalamu huenda hayo matokeo hasi yasingekuwapo.

Naujadili uongozi kuzaa utawala na jinsi ombwe la kukosekana uongozi linavyoweza kuathiri mambo mengi, ama kukwamisha mazuri yaliyokusudiwa na papo hapo kusababisha matokeo mabaya yasiyotarajiwa.

Tujikumbushe yaliyomtokea Nabii Musa baada ya kuwatoa ndugu zake kutoka kwenye mfumo wa ukandamizaji nchini Misri.

Siku moja mkwe wake aliyeitwa Yethero, alimwona Musa akizungukwa na watu kuanzia asubuhi hadi jioni, Yethero akamwambia Musa unachokifanya siyo sahihi ukiendelea hivi utadhoofu wewe na watu wote, akimaanisha litadhoofika Taifa zima la Israeli. 

Yethero akashauri akisema, “Jipatie watu waaminifu, walio wakweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu, waliojaa roho (hapa sifa za roho zinajulikana upendo, utu wema, uvumilivu, huruma, uadilifu  n.k) ukawaweke wawe wakuu wa maelfu, wakuu wa mamia na wakuu wa hamsini ili waamue kwa niaba yako na lile litakalowashinda ndilo wakuletee wewe kulitolea uamuzi wa mwisho.” 

Musa alikubali shauri hilo likaingizwa kwenye mfumo wao wa sheria ulioitwa Torati na ndilo lililozaa Baraza la wenye hekima sabini, ambalo baadaye Waisraeli waliita “Sanhedrin.” 

Kiongozi yeyote makini aliyedhamiria kufanikiwa lazima aunde jopo la uongozi unaotokana na watu makini wenye sifa sita alizoelezwa Nabii Musa, pia awe na utaratibu wa kuwafundisha hao wateule wake somo la uongozi, kwa sababu kila watakakokwenda hao anaowateua watamwakilisha Rais katika kuongoza watu. Ipo tofauti kubwa kati ya kuwaongoza watu na kuwatawala.

Kiongozi mkuu akipotoka akawateua watu kwa kutumia vigezo vingine kama urafiki na kujuana, ama akafanya uteuzi wake kwa kuzingatia wateuliwa wanavyomshabikia na wanavyomtii, atajikuta aidha amejiundia timu ya washabiki ama kundi la ‘loyalists’ wake wenye sifa moja tu kwamba wanamtii kwa mambo yote na ni watu wasiojua kumwambia hapana kwa lolote analotaka lifanyike. Hao watamwachia afanye hata lile wanaloona dhahiri kuwa halifai na litaleta madhara.

Tatizo jingine Rais akizungukwa na ‘loyalists’ hatimaye anaweza kujikuta akikasirishwa mara kwa mara na matokeo asiyoyatarajia, kwa sababu ataagiza mambo yanayotakiwa yafanyike kitaalamu nao ‘loyalists’ watayafanya kama anavyotaka ama watafanya kama anavyosema, badala ya kufanya kama inavyotakiwa hali hiyo itatoa matokeo hasi.

Rais atajikuta akisema mengi mazuri kwa wananchi anaowaongoza, lakini mazuri yote anayosema mdomoni yakiwa hayatafsiriki kimatendo. 

Rais aliyewasambaza ‘loyalists’ wake kila sehemu, atasema na wananchi juu ya mazuri yasiyozaa matunda mazuri, kwa sababu uongozi mzuri ndiyo unaozaa utawala makini. 

Kwa kuwa uongozi ni somo linalojitegemea, kiongozi mzuri huandaliwa na kutengenezwa, hata Nabii Musa pamoja na Mungu kumjaalia karama ya uongozi lakini bado alimpeleka darasani kujifunza a, b, c, d za uongozi. Nabii Musa alikuwa msomi kiwango cha shahada, maana nchini Misri ndiko ilikoanzia ‘university’ ya kwanza ulimwenguni. Hata wanafalsafa wa kale walitoka Ugiriki (Ulaya) na kwenda kusoma Misri (Afrika). 

Nabii Musa na elimu yake ya chuo kikuu bado Mungu alimsukumizia nchi ya Midiani akawa mchungaji wa kondoo kwa miaka arobaini. Katika kipindi hicho alijifunza uchungaji maana baadaye alitumia kanuni zile zile za kuchunga kondoo katika kuwaongoza watu akawachunga kwa miaka arobaini wakiwa safarini kuvuka jangwa kuelekea nchi ya ahadi.

Marais wengi walioongoza nchi zao kwa ufanisi, ni wale waliojiepusha kuwateua marafiki zao au ndugu wa karibu kwenye nafasi za uongozi. 

Uongozi wanchi unafanana na biashara hautaki ushemeji, udugu wala kujuana, yule anayeruhusu udugu, ushemeji, urafiki na kujuana ana nafasi kubwa ya kuangusha biashara yake kuliko yule atakayeweka watu wa mbali watakaojua fika kwamba uhusiano wao na mkubwa unaanzia na kuishia kwenye masuala ya kikazi tu na siyo masuala mengine.

Heri Rais yule anayeteua anaowachukia na kuwapa nafasi kulingana na uwezo wao kwa sababu yule anayejua fika kwamba ‘Bwana mkubwa’ anamchukia na anamwinda japo kwa kosa dogo tu ili apate fursa ya kumwadhibu, anaweza kufanya kazi na kutimiza majukumu yake vizuri kuliko yule anayejua fika hata akivurunda Rais hana cha kumfanya kutokana na wanavyofahamiana kwenye mambo mengine.

Rais akijihadaa kuteua anaowapenda tu, lakini wasio na uwezo wala sifa zinazotakiwa,wananchi walio chini yake wataendelea kuonja matokeo mabaya chini ya Rais wao wanayemwamini ni mtu mwema na mwenye mipango mingi mizuri.

Wananchi hawatajua ni wapi wema wa Rais wao unapopotelea na wapi mipango yake mizuri inapotibuliwa hadi kuwasababishia wao matokeo mabaya yanayowaumiza.

Rais akiwa na jopo la walaji rushwa, ama watu wasemao uongo wanaoogopa kumwambia bosi wao ukweli kwa hofu kwamba watamkasirisha, watu wapendao mapato ya vificho na wasiochukia mapato ya udhalimu, siku zote Rais atalaani rushwa lakini atajikuta rushwa na aina nyingine za ufisadi vikiongezeka siku baada ya siku chini ya utawala wake. 

Kwa sababu Rais pasipo kujua atakuwa amejiundia baraza la walazimishaji wasiokuwa na sifa ya kuongoza watu, hao walazimishaji wasiojua kuongoza watategemea utekelezaji wa mipango mingi mizuri ya Rais kwa njia ya ulazimishaji utakaofanya mazuri yote yaharibike.

Rais akikosa watu walio ‘wakweli’ na ‘wahalisia’ yaani ‘realistic’ siku zote atalishwa uongo, watu walio karibu naye watabaki na kazi moja tu ya kuisoma akili yake na kutafuta maneno yatayompendeza na kumburudisha ayasikiapo masikioni mwake. Lakini mwisho wa yote ni kushindwa kwa mipango yote licha ya uzuri wa mipango yenyewe.

Hatimaye Rais atajikuta akisomewa risala ndefu kila anapotembelea, atapewa sababu nyingi zilizoleta hali ya kushindwa, mwishowe naye Rais atajikuta anaishia kutoa hotuba za kuhalalisha kushindwa ama kukwama kwa utawala wao. Rais atajikuta akitumia nguvu za hoja kuwashawishi wananchi nao wakubaliane na sababu zilizoifikisha nchi yao kwenye hali ya kushindwa.

Masuala ya siasa safi, uongozi bora na utawala makini ni kama mnyororo ulivyoshikamana, yanahusiana na kutegemeana kama yai na kuku. Kwamba kuku anataga mayai na mayai yanaangua ama yanatotoa vifaranga, vivyo hivyo siasa safi inazaa uongozi bora nao uongozi bora unazaa serikali makini inayotawala kwa umakini.

 

>>ITAENDELEA 

By Jamhuri