‘Serikali ikiendeshwa kisiasa, CCM

ikiongozwa kiserikali Tanzania itadidimia’

 

Hii ni sehemu ya mwisho ya mada ihusuyo mambo yanayoweza kumkwamisha Rais Magufuli. 

Namshauri Rais na washauri wake wa kisiasa na kiserikali wajipatie vitabu viwili – cha ‘Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka’ wasome mada ya ‘Urais kiti cha moto’, humo nimefafanua historia ya taasisi yetu ya urais na magumu waliyoyakuta marais watatu waliotangulia – Julius Nyerere (1960-1985), Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) na Benjamin Mkapa (1995-2005).

Wakisoma wanaweza kuambulia chochote kuhusu matatizo ya kurithi yanayotoka utawala uliopita, matatizo sugu yanafanana na ugonjwa. Mtu anayetibiwa na anayemtibu wakiujua ugonjwa huwa hatua chanya kuelekea uponyaji, lakini anayeumwa na anayetibu wasipoujua ugonjwa huongeza ugumu katika kutibu.

Wataalamu wanasema ‘wrong treatment’ huchangia kuua wagonjwa wengi. Kihistoria ugonjwa wa malaria uliisumbua Dola ya Rumi kwa miaka mingi, neno ‘mala’ linalomaanisha mbaya na ‘aria’ linalomaanisha hewa au anga, yanathibitisha Warumi waliamini mtu anaugua baada ya kuvuta hewa chafu kando ya bahari. Hadi walipogundua kuwa unasababishwa na mbu, tayari malaria ilikuwa imewaangamiza mamilioni ya Warumi.

Nawashauri wasome kitabu kingine kiitwacho’Yes Mr Minister’ kilichotungwa na Waingereza, hukitumia kama mwongozo kila anayeajiriwa serikalini hutakiwa asome ili kimsaidie anapotimiza majukumu ya kiserikali ajue jinsi ya kuchukuliana na wanasiasa wanaokwenda serikalini. 

Siku nyingine nitajadili siasa za dola, leo nieleze kifupi kwamba iko tofauti kati ya vyama vya siasa (political parties) na siasa za vyama (party politics) ambazo zinatofautiana na siasa za dola (state politics).

Uongozi ukikosea ukachanganya mambo, ukazipeleka siasa za chama kinachotawala kwenye dola, na siasa za dola ukazipeleka kwenye chama ama kwenye vyama vya siasa vya upinzani, huo mkorogo utazaa mambo mapya na matatizo ya kutengenezwa.

Kwa sababu serikali itaendeshwa ‘kisiasa’na chama kinachotawala kitaongozwa ‘kiserikali’, hiyo ‘vice-versa’ ina athari nyingi (impact) zitakazokwamisha ufanisi wa serikali na hicho chama cha siasa kilichounda serikali.

Tanzania ina tatizo la kikatiba linatokana na ukweli kwamba nchi ilipoukubali mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, hayakufanyika mabadiliko makubwa ya kikatiba ili kurekebisha mambo ya msingi.

Utawala wa wakati huo ulifanya hila badala ya kuruhusu mageuzi ya kimfumo, ulinyofoa kifungu cha Katiba kilichozuia uwepo wa vyama vingine vya siasa ukaruhusu vianzishwe vyama vipya huku mfumo wa chama kimoja ukiendelea kubaki ulivyokuwa awali. 

Matokeo yake vyama vipya vilianzishwa na kuendeshwa ndani ya mfumo wa chama kimoja, huku CCM ikiendelea kuwa chama cha kidola kinachoendesha siasa kikiitumia dola. Ndiyo maana Jaji Mkuu, ama Mkuu wa Majeshi (CDF) au Mkuu wa Polisi (IGP) anaweza kugombea urais ama ubunge kwa tiketi ya CCM. Haulizwi (habanwi) aoneshe kadi yake alijiunga lini na chama cha siasa hadi kimwamini kugombea nafasi anayoitaka, wala haulizwi kama imani yake ya kisiasa ya chama anachogombea haikuathiri utendaji wake alipokuwa akiitumikia Serikali.  

Watendaji serikalini wanapoitumikia kwa siri siasa ya chama kinachounda serikali, wanaifanya serikali isiwatendee haki raia wote kwa usawa pasipo ubaguzi wala upendeleo.

Ubaguzi ni ubaguzi tu – ukifanywa katika misingi ya rangi utaitwa ‘racialism’ kama ile ‘apartheid’ ilivyoendeshwa na dola ya makaburu Afrika Kusini, ukifanywa katika misingi ya dini utaitwa ‘udini’na ukifanywa katika misingi ya kikabila utaitwa ‘ukabila.’ Katika Tanzania ubaguzi ukifanywa katika misingi ya tofauti za chama utaitwa ‘uchama’ huo utasababisha wananchi wanaobaguliwa waongeze chuki kwa serikali inayopendelea na CCM inayopendelewa.

Kwa sababu ubaguzi ni dhambi ileile yenye athari zilezile, Mwalimu Nyerere aliuita ‘ukaburu’ akamfananisha mbaguzi na anayekula nyama ya mtu, akasema aliyeonja nyama ya mtu haachi. Dhambi ya ubaguzi huwatafuna hata hao wanaowabagua wenzao, serikali ikiendesha ubaguzi wa kichama, ikaonesha wazi kwamba ina chama chake, haitaishia hapo tu kumiliki au kumilikiwa na chama, bali itasogea hatua nyingine zaidi. 

Kwa kuwa vyama vingine vipo, serikali itajikuta ikivipinga vyama vinavyopinga chama chake, ama itapambana na wapinzani ili kuhami maslahi ya ‘kichama’ ambayo kimakosa yatanasibishwa na maslahi ya taifa.

Watanzania tuna tatizo la pili. Nimelieleza kwenye maandiko yangu mengi. Rais wetu ni mkuu wa dola, kiongozi wa Serikali iliyo madarakani pia anaongoza chama cha siasa. Hali hiyo inafanya Tanzania ijiendeshe tofauti na Uingereza tulikorithi utawala wa kikatiba na mfumo wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi hatimaye vinaunda serikali. 

Nchini Uingereza, Waziri Mkuu haongozi chama cha siasa wala mfumo wao haumgeuzi mateka wa chama kilichomdhamini.

Watanzania tunaendesha mambo yetu tofauti na Marekani tulikoiga na kudakishwa (adopted) mfumo wa rais mtendaji ‘Executive President.’ Nchini Marekani, rais haongozi chama cha siasa wala hajishughulishi kabisa na siasa za vyama (party politics), anajishughulisha na siasa za dola (state politics) ili kulinda maslahi ya kudumu ya taifa la Marekani.

Utaratibu wetu unaomfanya Rais awe kiongozi wa chama cha siasa pia awe kiongozi wa Serikali, tumedumu nao tangu enzi za mfumo wa chama kimoja. Wakati huo hayakuonekana matatizo tuyaonayo sasa kwa sababu havikuwako vyama rasmi vya upinzani. 

Mfumo wa chama kimoja uliibadilisha sura ya upinzani ukaugeuza ‘ukosoaji’, ikaelezwa bayana kila ‘mwanaCCM’ awe tayari kujikosoa mwenyewe na akubali kukosolewa. CCM iliukubali utaratibu wa wanachama na viongozi kukosoana, lakini mazuri hayo sasa hayapo.

Kuna ugumu wa kuendelea nayo chini ya mazingira ya uwepo vyama vya upinzani, vyenye haki ya kufanya yote mawili yaani kuwakosoa viongozi wa Serikali, kukosoa siasa za dola na kukipinga chama kinachotawala. 

Sasa haitatokea kada wa CCM kuukosoa uongozi wa CCM ama kuikosoa Serikali wala kuzikosoa siasa zinazoendesha dola, anahofia kuonekana msaliti ama anayeimba wimbo wa wapinzani.

‘WanaCCM’ kukosoana ni utamaduni mzuri uliopotea mwaka 1992 ulipoingia mfumo wa vyama vingi, sasa kada wa CCM anapaswa kuitetea CCM yake hata pale yanapoonekana wazi mabaya yanayoathiri maslahi ya Taifa. Kwa sababu hakuna ‘mwanaCCM’ aliye tayari kuonekana amevaa joho la upinzani wala aliye tayari kuonekana msaliti.

Ukweli ni kwamba demokrasia ya chama kimoja iliuawa na ujio wa vyama vingi na nafasi yake ikachukuliwa na udikteta wa vyama vya siasa ambao hayati Mummar Gaddafi alisema ni mbaya kuliko udikteta wa kijeshi. 

Vyama vinawaburuza wanachama, hakuna demokrasia ndani ya vyama hata hivyo vya upinzani vinavyojifanya kuipigania demokrasia. Ndani ya vyama kuna udikteta wa kutisha, ndiyo maana kiongozi mkuu wa chama ama kamati kuu ya chama au baraza kuu, yaani kundi dogo la watu 20 au 40 wanaweza kukurupuka na kuamua kuandamanisha watu nchi nzima.

Hawajali kuwashirikisha wanachama ili walau kupata mawazo yao au maoni tofauti. Viongozi wanawaona wanachama kama ‘roboti’ wanaotakiwa kupokea maagizo yatokayo juu na kuyatii. Vyama vya siasa vimejiumbia utamaduni wa kutiririsha mambo kutoka juu kwenda chini, havina utaratibu wa kupokea kutoka chini kwenye matawi kupeleka mambo juu hadi uongozi wa kitaifa. 

Mfumo huu hauliwezeshi kundi dogo lililo juu kupata wala kupokea mawazo mapya, viongozi walio juu wamechukuliwa kijumla kwamba daima wako sahihi hawahitaji maoni wala mawazo ya wanachama na wananchi wengine kiujumla. Matokeo yake viongozi wa juu wanaishi tofauti na uhalisia, wanashikilia mambo mengi ya kufikirika yasiyo halisi.

Kwa sasa Rais kuendelea na kofia mbili ni tatizo kwa sababu anafanana na mungu wa Kirumi aliyeitwa ‘Janus’ aliyeadhimishwa mwezi Januari aliyekuwa na nyuso mbili bila kisogo.

Ninaposema rais simaanishi Magufuli, namaanisha hata akiwa Mbowe au Seif, bado chini ya mfumo chotara tulio nao sasa rais akitoa kauli haijulikani wakati gani anasema kama kiongozi wa chama cha siasa anayestahili kupingwa na wakati gani anasema kama mkuu wa dola asiyestahili kupingwa.

Haitawezekana Tanzania ziweko haki mbili zinazokinzana kwa wakati mmoja, yaani haki inayowaruhusu Watanzania kumpinga rais wao anapotoa kauli za kisiasa, kwa sababu anaongoza chama cha siasa na haki ya rais kutokupingwa na Watanzania asemapo kama mkuu wa dola kwa kuwa dola haina mpinzani (serikali haitakiwi ipingwe).

Hayo mawili yaani uongozi wa chama na ukuu wa dola yasipochanganuliwa yakawekwa wazi na kueleweka kwa Watanzania wote, yataendelea kuchanganya kama huo mkanganyiko ulioonyeshwa na utafiti wa ‘TWAWEZA’. 

Kulingana na ‘TWAWEZA’, wapo Watanzania wanaomwona Rais ni dikteta, kwa sababu kauli zake hazipingwi ila wengine wanamwona ‘mwajibikaji’ kwa sababu anapoongoza chama, anatimiza wajibu wake kichama na lazima afanye shughuli za kisiasa.

Mtu mmoja anaposhikamanishwa yote mawili, uongozi wa chama unaomlazimisha aendeshe shughuli za kisiasa na kazi za chama, kuna wakati atalazimika kutetea chama chake. Mtu huyo mmoja anatakiwa afanye shughuli za kiserikali, kuna wakati analazimika kutetea siasa za dola zinazolinda maslahi ya Taifa, anaweza kujikuta akichanganya ‘uchama’ serikalini ama akachanganya ‘userikali’ kwenye chama chake.

Nimemkumbuka hayati Mashaka Nindi Chimoto, aliyekuwa kada wa CCM baadaye tukawa naye kwenye harakati za mageuzi, Nyerere alipokuwa Rais Chimoto akiwaseminisha wakuu wa wilaya, alisema maneno mengi ya hovyo dhidi ya Nyerere. Mtu mmoja akampigia simu Nyerere akamwambia leo “Umetukanwa sana na Chimoto, alikuja amelewa.” Chimoto alijitetea kwamba “Nimemtukana Nyerere kichama siyo kiserikali.” Mashauri yake yakapelekwa kumalizwa kwenye chama siyo serikalini. Chimoto hakupandishwa kizimbani kujibu shitaka la kumkashifu Rais Nyerere.

Mwaka 1997 nilipokuwa nikienda New York, nilipitia London kwenye ofisi ya chama cha Labour ili kumwandalia ‘appointment’ aliyekuwa Mwenyekiti wetu, Augustine Mrema, aonane na Tony Blair. 

Mwanamama Sigler aliyekuwa akishughulikia mambo ya nje ya chama cha Labour, akaniambia hata sisi tunapotaka kumwona Antony kama Waziri Mkuu huwa tunalazimika kuomba ‘appointment’ serikalini. Mbinu tunayotumia huwa tunaandaa ‘tea party’ na kumwita kama mwanachama, ndivyo alivyoonana na Raila Odinga, Mwai Kibaki, Kenneth Matiba na wengineo, labda tufanye hivyo kwa Mrema. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia Antony nikajua kumbe tunapoita Tony huwa tunafupisha jina lake.

Nchini Uingereza, serikali ni ya wananchi wote, haijabinafsishwa kugeuzwa mali ya chama kilichounda serikali. Waziri Mkuu wao anahesabiwa ni mali ya Waingereza wote siyo mali ya chama, lakini kwetu Rais amenasibishwa chama, na Serikali imeungamanishwa na chama cha siasa, umetengenezwa mgogoro unaoipunguzia Serikali uhalali wa kuheshimiwa na wote.

 

>>TAMATI>>

3310 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!