Kwa mwezi mzima sasa Taifa letu limegubikwa na vurugu za umiliki wa gesi. Wakazi wa Mkoa wa Mtwara wakiongozwa na propaganda za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye sasa anazungumza lugha za malaika akidai anawatetea wananchi wa Mtwara, wanachimba mtaro kwa ajili ya mkondo wa maafa.

Najua mara nyingi katika mazingira ya sasa watu wamejaa upepo. Inawezekana hata uwezo wa kufikiri kwa baadhi ya watu umeshashuka, hivyo hata ninavyoandika makala haya jibu la kwanza litakuwa ni kutukanwa badala ya kuangalia mantiki ya hoja.

 

Nasema hivi baada ya kushambuliwa kiasi cha kutosha wiki mbili zilizopita, nilipoandika makala ya kupinga nia ya wakazi wa Mtwara. Nimejifunza jambo.


Wiki hii Zitto amesambaza ujumbe, kama kawaida yake, maana siku hizi ‘amehitimu’ uandishi wa habari. Akiandika taarifa kwa vyombo vya habari (press release) anaweka hadi kichwa cha habari na kuvisukumia vyombo vya habari vichapishe. Nasema kwa uzuzu wa baadhi ya vyombo vya habari vinachapisha vilevile maneno ya Zitto bila kuyahariri.


Nasikitika kuandika haya, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimepoteza sifa ya kuitwa vyombo vya habari. Kazi ya Mhariri ni kuhariri kinachoingia gazetini, redioni au kwenye televisheni kwa nia ya kuangalia maslahi mapana ya jamii badala ya vikundi vya watu. Vyombo vya habari vipo kutumikia maslahi ya jamii (public interests) na si matakwa ya jamii (interests of the public).


Wahariri wanapaswa kufahamu kuwa wana majukumu ya kitaaluma ya kutanua (expanding) ikiwa habari husika ina upungufu, kupunguza (limiting) ikiwa imepitiliza kiwango – (hii ni pamoja na kuondoa matusi, uchochezi na maneno yanayoweza kuleta hatari kwa jamii) – kuiwasilisha ilivyo (relaying) ikiwa habari haina matatizo au kutafsiri (interpreting) ikiwa habari haieleweki.


Wiki iliyopita nilipata barua pepe (e-mail) ya Zitto yenye kichwa cha habari kinachosema: “Mtwara: Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza wananchi.” Kwa ufupi inahanikiza watu wa Mtwara kutoisikiliza Serikali akidai haina uwezo wa kulinda bomba la gesi. Baada ya kusoma barua ya Zitto nilimjibu hivi:-


“Zitto, hakika katika hili wewe ndiye hasa unayefanya kazi ya kugawa nchi. Kumbuka mchango na maelezo yako juu ya suala la Bulyanhulu na Dowans ulivyokuwa ukitanguliza na kutetea masilahi ya Taifa.


“Kwa masikitiko leo unatetea masilahi ya vikundi? Tena bila aibu unafanya uchochezi eti Serikali haiwezi kulilinda bomba la gesi kwa maana unawaelekeza walihujumu?


“Ndugu yangu, think beyond politics. Leo unathubutu kutetea elements za uasi za kuanzisha Jamhuri ya Makonde? Ukiambiwa unatumiwa uchukie? Hii ni aibu. Piga moyo konde, fikiria Taifa katika umoja wake.


“Waeleze wananchi ukweli wote, si nusu ukweli. Waeleze gharama za kujenga gridi, na ukweli kwamba zaidi ya umeme, gesi inakwenda Dar kutumika viwandani, majumbani na kwenye magari.


“Waambie wananchi kuwa Somanga Fungu (Lindi) utajengwa mtambo wa kuzalisha megawati 520, na Mtwara vinajengwa viwanda vya mbolea na LPG.


“Kwa nini husemi ukweli huu? Mimi niko wazi katika hili la Mtwara kuwa umenikera na ikibidi nitaamua kwenda public kukupinga kwa uwazi maana unapalilia uasi katika nchi.

“Balile.”


Nimeona mchezo huu unaendelea na nimeamua kwenda public. Kabla ya barua ya Zitto, nilipokea ujumbe kupitia simu yangu uliotoka Namba 0656 694015, ambaye alikataa kunitajia jina lake, lakini kwa mujibu wa usajili, simu hii inamilikiwa na mtu anayeitwa FARAJI HASANI ukisema:


“KUANZIA JIWE LA MZUNGU KILWA HADI MSIMBATI UNAPOISHIA MTO RUVUMA NA BAHARI YA HINDI, NANYUMBU, LIWALE HADI KINJUMBI – INATOSHA KUWA NCHI KUBWA KULIKO BURUNDI, RWANDA, MALAWI, CAPE VERDE, BOTSWANA NA ZINGINE. TAIFA LETU NI REPUBLICA DE MAKONDE LAND. TUPELEKE MAOMBI YA KUJITENGA UMOJA WA MATAIFA TUWE NCHI HURU KUSINI TOKA ZAMANI TUKO NYUMA YA PAZIA. KUNJA PAZIA LIWALO NA LIWE WAO WAO, SISI KWA SISI. MBONA SUDANI WAMEWEZA KUGAWANA NCHI? JIONI NJEMA.”


Ujumbe huu ulinifikia saa 03:05:39 usiku. Ilikuwa Alhamis, Januari 10, 2013. Hakika sikupata usingizi hadi saa 09:00 alfajiri. Niliamka nikaandika sehemu ya makala haya. Nilitaka niyatumie wiki iliyopita, nikasitisha kidogo, lakini nadhani ni mwafaka kuyatumia wiki hii. Imeniogopesha. Nimepata hofu ya kutisha. Nimebaini kuwa kumbe ajenda si gesi, bali kuna lao jambo.


Namba hiyo hiyo, siku tano baadaye, yaani Januari 15, 2013 ikaniletea ujumbe niliouelewa vyema. Nikaelewa machungu wanayopata wananchi wa Mtwara kuona wanaachwa nyuma kimaendeleo. Ujumbe wake ulisema hivi:-


“(A) CCM imeng’oa mashine ya maji Newala Kitangili wakapeleka Dodoma, tumewavumilia, ambayo ilikuwa ya msaada kutoka Finland. (B) CCM wamepindisha kiwanda cha samaki kujengwa Mtwara wakapeleka Dar es Salaam, tumewavumilia. (C) CCM wameng’oa taa za mwanga mkali za Uwanja wa Ndege Mtwara wakapeleka Arusha, tumewavumilia. (D) CCM imeng’oa reli kupeleka Dar es Salaam, tumewavumilia.


“(E) CCM imepindisha mkataba wa kutumika kwa Bandari ya Mtwara na Malawi kibiashara, wakapeleka Bagamoyo, bado tukawavumilia, leo hii wanataka kutoa gesi tena wanapeleka Dar es Salaam??? Eeee! Imefika wakati sasa tuseme inatosha. Asitushinde. Je, hayo yote yamesababishwa na historia?”


Narudia. Nayaelewa machungu ya watu wa Mtwara. Tatizo linajitokeza tunapoanzisha utaratibu wa kila mtu kusema kilichopo kwake ni chake. Zanzibar wamekuwa wakisema mafuta ni yao tunapiga kelele. Hamisi Kigwangala alianzisha hoja kuwa madini yanayopatikana Nzega yawafaidishe wao, tukashangilia.


Sasa tulipofika siko. Ruvu wakisema maji yao yasipelekwe Dar es Salaam; Mwanza na Shinyanga nao wakasimama kudai kuwa dhahabu na almasi vinavyochimbwa huko visipelekwe Dar es Salaam; Tanga nao wakasema umeme wao usipelekwe Pemba; Dar es Salaam nao wakasema wagonjwa kutoka mikoa mingine wasiletwe Hospitali ya Muhimbili, Hindu Mandal au Aga Khan; Bukoba, Mwanza na Mara wakasema samaki wao wasipelekwe Ulaya, na wengine hivyo hivyo na wakafanikiwa. Hii itakuwa hatua ya mwanzo.


Hatua itakayofuata, kila mkoa utasema Serikali Kuu isitoze kodi watatoza wao, kinachopatikana watatumia mikoani kwao. Nasema ikiwa utaratibu ndiyo huu, basi kila mkoa, wilaya, kata, kijiji na kitongoji kitajitangazia Jamhuri yake. Ni kwa mwelekeo huu nasema tunachimba mtaro wa kuigawa nchi vipande.


Zitto anaweza akawa anatafuta umaarufu wa kisiasa, lakini pia inawezekana alikuwa bado ananyonya wakati tunapigana vita na Uganda. Angetuuliza sisi tuliokuwa shuleni tumweleze tulivyolazimika kuchimba handaki.


Suala hili linaweza kuchukuliwa kama gesi, lakini kwa maandishi na matamko ya Zitto na wengi wenye mtazamo kama huo, nchi yetu ikiwasikiliza inaandaa mazingira ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.


Na hili nasema tutajuta mbele ya safari. Hakika tuzipuuze siasa za akina Zitto kwenye suala hili la gesi. Mungu ibariki Tanzania.


By Jamhuri