Mdemu awataka wanawake kupeana sapoti na kushikamana katika fursa zinazotolewa na Serikali

Na WMJJWM – Iringa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, ametoa wito kwa wanawake nchini kupendana, kushikamana, na kupeana taarifa kuhusu fursa zinazotolewa na serikali ili kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali za kijamii na kisiasa, ikiwemo kugombea nafasi za uongozi.

Mdemu ametoa kauli hiyo Juni 22, 2025 wakati wa hotuba yake kwenye kongamano la kuelekea kilele cha Siku ya Wajane na Wagane Duniani, linalotarajiwa kufanyika Juni 23, 2025, mkoani Iringa.

Katika hotuba hiyo, amesisitiza umuhimu wa wanawake kuelimishana na kupeana taarifa kuhusu mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kama njia ya kuwawezesha kiuchumi.

“Kinamama tupendane, tuache chuki na wivu wa maendeleo. Tushikane mikono, tupeane fursa. Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupatia mikopo na fursa nyingi kwa ajili ya kutuinua kiuchumi. Naomba tupeane habari na tushirikiane kuzifikia, tuache kukwamishana,” amesema Mdemu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunur, ametoa pongezi kwa uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuandaa kongamano hilo muhimu ambalo limewakutanisha wajane na wagane ili kujadili changamoto na fursa zinazowahusu.

“Ni faraja yetu kukutana nanyi leo, na tumeweza kujifunza mambo kadhaa. Tuna matumaini kuwa mtayafanyia kazi mafunzo mliyopata ili yakawasaidie kukabiliana na changamoto na kukimbilia fursa mbalimbali. Serikali imeendelea kupokea na kutatua changamoto za makundi maalum, ikiwemo wajane na wagane,” amesema Badru.

Aidha, Afisa Maendeleo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni amewataka wanawake kuwa na nidhamu ya fedha na kujifunza tabia ya kujiwekea akiba, hata kama ni kidogo, ili waweze kujitegemea kiuchumi. Pia aliwasihi kusimamia kwa uadilifu mali walizoachiwa na wenza wao waliotangulia mbele za haki.

Baadhi ya wajane na wagane walioshiriki kongamano hilo waliishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuwaandalia siku maalum inayolenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.