Na Mwandishi Wetu, JmahuriMedia, Morogoro
Wakulima wameshauriwa kujenga tabia ya kupima afya ya udongo kwa ajili ya kujua aina ya virubutisho vilivyopo kwenye udongo kabla ya kuanza kutumia mbolea.
Ofisa Ugani wa Minjingu Mines & Fertilizer Ltd Tanzania, Franks Kamhabwa alitoa ushauri huo kwa wakulima waliotembelea banda la Kampuni hiyo katika maonesho ya Nanenane ya Kanda ya Mashariki kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro.
Kamhabwa amesema mmea ni kiumbe hai ambacho kinahitaji virutubisho vya aina moja au nyingine kwa hivyo ni vyema wakulima wakajenga tabia ya kupima udongo ili kutaka kujua ni kiasi gani cha kirutubisho kinachohitajika katika udongo kwenye eneo husika la uzalishaji.
“Unapopata matokeo ya nini kinatakiwa kwenye udongo halafu ukajua ni mmea gani utakwenda kuupanda hapo maana yake sasa unaweza kujua ni aina gani ya mbolea inayohitajika kutumika“ amesema Ofisa Ugani Kamhabwa,” amesema.
Kamhabwa amesema kuwa bila ya kupima afya ya udongo ,wakulima watakuwa wanatumia mbolea kiholela basipo kuwa na uhakika ya kwamba anachokifanya ni tofauti na matarajio uzalishaji wenye kuzingatia tija.
“ Rai yangu ni kwamba wakulima waendelee kupima afya ya udongo ili kuwa na uhakika wa kufanya kilimo endelevu , kilimo chenye tija ili tuweze kupata usalama wa chakula pamoja na kipato” amesema Kamhabwa.
Wakati huo huo ,Mtaalamu Mwandamizi wa Maabara kutoka Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Hellen Kanyagha amesema kuwa wakulima wanaolenga kilimo chenye tija ni vyema wahakikishe wanapima afya ya udongo pamoja na afya ya mbegu ili kuepuka hasara na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Dk Kanyagha amesema hayo katika Banda la Chuo Kikuu hicho alipokuwa akitoa elimu kwa wakulima juu ya huduma ya upamaji wa udongo, afya ya mimea na mbegu.
“Kwanini ni muhimu mkulima kupima udongo, kwa sababu inamsaidia kufahamu kiasi cha virutubisho kilichopo katika udongo”amesema
“ Pia inampa uwezo wa kujua aina ya mbolea anayotakiwa kutumia na aina gani ya virutubisho vinatakiwa kuongezwa kwenye udongo wake ili aweze kulima kwa tija na kupata mazao bora na yenye afya bora,” amesisitiza Dk Kanyagha.
