Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
WATANZANIA na wawekezaji nchini wametakiwa kujitokeza kuchangamkia fursa zinazotokana na zao la mkonge, baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya mbegu, mitambo ya usindikaji na bidhaa zinazotokana na zao hilo.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Simon Kibasa, amesema sekta hiyo kwa sasa imepiga hatua kubwa kibiashara na kuibua mahitaji makubwa sokoni.
“Kwa sasa, mahitaji ya mbegu za mkonge kitaifa ni zaidi ya milioni 60, wakati uzalishaji uliopo ni milioni 25. Hii inamaanisha kuna pengo la mbegu milioni 35, ambalo linaweza kuzibwa na wawekezaji wapya,” amesema Kibasa.
Kwa mujibu wake, uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 39,000 mwaka 2020 hadi tani 61,000 mwaka 2024, huku idadi ya wakulima ikiongezeka kutoka 7,551 hadi 20,000 katika kipindi hicho.

Kibasa amebainisha kuwa pamoja na uwekezaji wa serikali kwenye mitambo ya usindikaji, bado kuna uhitaji wa zaidi ya mitambo mikubwa 25 ya kusimika mkonge.
Aidha, alitaja fursa nyingine kuwa ni biashara ya kuuza singa za mkonge ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza thamani kwa kutengeneza bidhaa kama vikapu, kamba na magunia.
“Tasnia ya mkonge iliporomoka kati ya mwaka 1984 hadi 2011 kutokana na ushindani wa bidhaa za plastiki, lakini sasa inapata uhai mpya kutokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa rafiki kwa mazingira, ikiwemo vifaa vya magari kama dashboard,” ameongeza.
Ametaja pia ubunifu mwingine katika sekta hiyo kuwa ni kuzalisha uyoga kwa kutumia mabaki ya mkonge baada ya usindikaji, akisema soko la uyoga ni kubwa na lenye faida.
Bodi ya Mkonge Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, inasimamia maendeleo ya zao hilo na inashiriki Nanenane ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika kilimo, biashara na teknolojia ya mkonge.