Na Aziza Nagwa, JamhuriMedia, Kisarawe

Shirika lisilo la kiserikali linalowasaidia wasichana kujiinua kiuchumi, INITIATIVE, limewapatia pesa na vifaa wasichana walio nje ya shule katika Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, ili waweze kujinufaisha kiuchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kisarawe, ambaye pia ni Ofisa Utamaduni, Venance Kihima, amesema shirika hilo limekuwa mkombozi kwa wasichana wenye hali duni kwa kuwasaidia kujiinua kiuchumi kupitia mradi huo.

Amesema mpango huo utawasaidia wasichana kuepuka kujiingiza katika
makundi mabaya na badala yake wajishughulishe na shughuli za uzalishaji mali ili kuboresha hali zao za kiuchumi.

Aidha amedai mpango huo utaweza kuwasaidia wasichana kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kutoka kwa wanaume na vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo ni muhimu kutumia fursa waliyoipata kwa njia bora ili kujikwamua kiuchumi.

“Mradi huu utakuwa msaada mkubwa wa kuinua familia masikini kwa sababu
wataweza kutumia mapato yao kuendeleza familia zao na kupata mahitaji muhimu” amesema.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Lydia Moyo, amesema tayari wameshawasaidia
wasichana zaidi ya 100 na wengine wamefikia hatua kubwa zaidi kwa kuanzisha biashara zaidi ya moja.

“Naamini kupitia mafanikio ambayo wameyapata wenzao kwa ushuhuda,
wataona kama chachu ya kuwafikia na wataweza kuiga mifano ya wenzao kwa kukuza mitaji waliyopata na kuongeza bidii ya kuanzisha zaidi,” amedai.

Lydia amesema shirika lao linajishughulisha na kuwawezesha na kuwasaidia wasichana kujiinua kiuchumi kwa kutumia uwezeshaji wa
kiuchumi na teknolojia.

Akifafanua zaidi, alidai kuwa shirika hilo limefika Kisarawe tangu mwaka 2019 kwa lengo la kuwasaidia wasichana walioko nje ya shule.

Baada ya kubaini hali hiyo, walikamua kuanzisha mradi wa Plan B, ambao
unamaanisha mpango wa pili baada ya wa kwanza kushindwa kuleta matokeo chanya kwa msichana kutokana na sababu mbalimbali.

Lydia amedai kwamba lengo la mradi huo ni kumrejeshea matumaini msichana aliyoyapoteza au kuyakosa, na kumfanya asonge mbele kupitia mpango huo.

Malengo mengine ya mradi huo ni kumfanya msichana ajimudu kiuchumi ili aweze kuepuka unyanyasaji wa kijinsia, kwa sababu msichana akielimika na kuwezeshwa kiuchumi, ni wazi atakuwa imara na hataweza kupitia ukatili tena kwa sababu anajimudu kiuchumi.

“Mradi huu umewalenga hasa wasichana ambao wapo nje ya shule waweze kutimiza malengo yao ya kutimiza ndoto zao. Kwa hiyo, tunachokifanya ni kuwawezesha kiuchumi kwa kuanza na kuwajengea uwezo wa elimu ya biashara, na mwisho kuwapatia mitaji ili waweze kuanzisha biashara mbalimbali katika maeneo yao,” amesema.

Aidha, amedai kuwa wasichana wengi wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia kwa sababu wanakuwa na mahitaji ya kiuchumi ambayo wanashindwa kuyamudu.

Ndiyo maana kama shirika, tumeona msaada wa kwanza kwao ni kuwapatia uwezeshaji wa kiuchumi kama njia ya kuwasadia kujilinda na ukatili wa kijinsia.

Amesisitiza Wasichana wasikate tamaa na kujingiza katika mazingira ya ukatili kwa sababu wana uhitaji wapaze sauti za kujitetea dhidi ya ukatili.

Kwenye kuendesha mradi huu, tumejifunza mengi,mwanzoni, tulikuwa tunawapatia pesa, lakini baada ya kuona hakuna uaminifu kwa baadhi, ndiyo maana tunawapatia vifaa na pesa ili waweze kwenda moja kwa moja kuanzisha biashara za kujinua kiuchumi katika maeneo yao.

Lydia amedai baada ya kuona kuna udanganyifu, walikamua kuwatumia maafisa maendeleo wa kata na wazazi wao kabla ya kuwapa msaada ili aweze kuwasimamia vizuri.

Amedai kuwa mpango huo mpaka sasa tayari umewawezesha wasichana zaidi ya 100, ambao wengine baada ya kuwawezesha wamefikia hatua kubwa ya kuanzisha zaidi ya biashara.

Mmoja wa washiriki, Salma Kambaulaya, amesema msaada huo wa kiuchumi
utamwezesha kuanzisha biashara ya mama lishe kwa sababu katika kijiji chao kuna uhaba wa mama lishe.

“Msaada huu umenikomboa mimi na familia yangu kwa sababu nitaweza
kuendeleza biashara kwa uangalifu ili niweze kufika mbali kiuchumi,” amesema.

Amewaomba wasichana ambao hawapo katika mpango huo wajitokeze
ili wawasaidie kujiinua kiuchumi na kusaidia familia zao.

Radhia Hamidu kutoka kikundi cha uzaaji wa viatu, pochi na madera amesema mradi huo umewafanya wajisikie vizuri kwa sababu wanakwenda kuanza maisha mapya na kutimiza ndoto zao.

Agness Steven, mwakilishi wa ofisa maendeleo ya jamii kata ya Masaki,
amesema anawashukuru shirika hilo kwa kuwatafuta wasichana ambao walikuwa katika mazingira magumu na kuwawezesha kiuchumi.

Amesema ni vyema wakatumia elimu waliyopata pamoja na uwezeshaji huo
kujiinua kiuchumi na familia zao, na kamwe wasirudi nyuma katika dimbwi la umasikini.