Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa watu wasio na makaazi lazima “waondoke” Washington DC huku akiapa kukabiliana na uhalifu katika mji huo.
Trump alitia saini amri mwezi uliopita ili kurahisisha kuwakamata watu wasio na makazi, na wiki iliyopita aliamuru utekelezaji wa sheria katika mitaa ya Washington DC.
Kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wake wa kijamii Truth Social siku ya Jumapili, Trump aliandika:
“Wasiokuwa na makazi wanapaswa kuondoka MARA MOJA.”
Aliendelea kwa kusema kuwa watu hao watapewa mahali pa kuishi, lakini mbali na mji mkuu.
Kwa upande wa wahalifu, alisema hawatabeba virago vyao bali watawekwa jela.
Trump alifuatisha ujumbe huo na picha zinazoonesha mahema na takataka mitaani.
Mpango huu mpya haujafafanuliwa kwa kina, lakini si mara ya kwanza Trump kulizungumzia suala la watu wasio na makazi.
Mwaka 2022, alieleza kuwa watu hao wanapaswa kuhamishiwa kwenye maeneo ya nje ya miji, wakipewa mahema ya kisasa pamoja na huduma muhimu kama vyoo na matibabu.
Lakini matamshi haya, japo yamepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wafuasi wake, pia yameibua hisia mseto kwa wengine hasa wanaoona kuwa watu wasio na makazi ni raia wanaokumbwa na changamoto halisi kama ukosefu wa ajira, afya ya akili, au matatizo ya kiuchumi, si wahalifu wala hatari kwa jamii.
Katika ujumbe mwingine, alimpongeza Meya Bowser kama “mtu mwema anayejitahidi,” lakini akasisitiza kuwa licha ya juhudi zake, mji unazidi kuwa “mchafu, hatari na usiovutia.”
Hata hivyo, Meya Muriel Bowser amekosoa hatua ya baadhi ya viongozi wa Ikulu ya White House kuwa DC ni hatari zaidi kuliko Baghdad, akisema kuwa kulinganisha mji wa Marekani na nchi iliyo kwenye vita ni jambo la kupindisha ukweli.
Meya huyo akizungumza na MSNBC, alisema “Ni kweli tuliona ongezeko kubwa la uhalifu mwaka 2023, lakini tangu wakati huo tumefanya kazi kubwa kuupunguza. Kwa sasa, tuna viwango vya chini zaidi vya uhalifu wa kutumia nguvu katika kipindi cha miaka 30.
Trump anatarajiwa kufanya mkutano na wanahabari katika Ikulu, ambapo atatoa mpango wa kukabiliana na uhalifu jijini.
Pia ametangaza kuwa atagusia mabadiliko ya kimazingira na ukarabati wa sura ya mji.
Kwa mujibu wa Community Partnership, shirika linalosaidia kupunguza ukosefu wa makazi, takribani watu 3,782 hulala bila makazi katika jiji kuu la Marekani kila usiku.
Kati yao, wengi wako kwenye makazi ya muda au nyumba za dharura, lakini takriban 800 wanalala wazi mitaani.
