Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Emmanuel Shindika, amewakabidhi bendera ya taifa wanamichezo wa Tanzania watakaoshiriki Mashindano ya Michezo ya Shule za Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA) 2025, huku akiwaasa kudumisha nidhamu, utulivu na mshikamano kipindi chote cha mashindano hayo.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi bendera hiyo, Dkt. Shindika alisisitiza kuwa wanamichezo hao wanabeba taswira ya taifa, hivyo wanapaswa kuonesha sifa kuu za Tanzania ambazo ni heshima, amani na mshikamano.
“Niwasihi mrejee na vikombe vingi ili tumthibitishie Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa tulistahili kushiriki mashindano haya,” alisema Dkt. Shindika.
Aidha, aliwataka kuongeza bidii katika michezo yao, akiwakumbusha kuwa kuibeba bendera ya taifa ni kuibeba nchi, na macho ya Watanzania yote yako kwao wakitarajia kuona wakifanya vizuri na kuibua heshima kwa taifa.
Kwa upande wao, wanamichezo hao walieleza kujiamini kuwa mwaka huu watafanya vizuri zaidi na kurejea na medali nyingi kuliko mwaka jana, ambapo walishiriki FEASSA nchini Uganda na kufanikwa kurejea na medali 58 pekee.
Wanamichezo hao wameondoka kupitia mpaka wa Sirari, mkoani Mara, baada ya kuweka kambi ya mazoezi kwa siku kadhaa katika Chuo cha Ualimu Tarime, wakijiandaa kushindana na wenzao kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kituo chao cha mashindano kikiwa Kakamega, Kenya.



