Na Hellen Mtereko,Mwanza

Jeshi la magereza Mkoani Mwanza limeeleza njia bora ya kuwaandaa wafungwa ili wawe raia wema uraiani ni kwa kuwajengea misingi ya stadi za kimaisha wanapokuwa magerezani.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Magereza Mkoani Mwanza, Masudi Kimolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo kwa lengo la kuwajengea maarifa ya stadi za maisha wafungwa.

Alisema katika magereza ya Mwanza kuna miradi ya kilimo cha bustani, ufugaji wa nyuki, kuku, ng’ombe, samaki wa vizimba na ushonaji wa vikoi ambapo vitu vyote hivyo vikimjenga mfungwa akiwa gerezani hupata maarifa yatakayomfanya akajitegemee vizuri baada ya kurudi uraiani.

“Tunawafundisha wafungwa wetu vilevile waweze kuwa marafiki wa mazingira kwa kupanda mazao kwenye mifuko inayotupwa na kutumia sehemu ndogo kwa kulima ” alisema Kimolo.

Kimolo alitoa wito kwa wafungwa kuwa na ari ya kujifunza mafunzo wanayopata kila siku ili yaweza kuwasaidia pindi watakapo hitimu kifungo chao na kwenda kuanza maisha yao majumbani kwao.