Marekani imeliwekea vikwazo kundi lenye silaha nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo linalofanya kazi na serikali ya Kinshasa, chama cha ushirika cha uchimbaji madini nchini humo, na makampuni mawili ya Hong Kong, ikiwatuhumu kuchangia ukosefu wa usalama nchini DRC na uchimbaji madini kinyume cha sheria.

Wizara ya fedha ya Marekani inasema inalenga moja ya makundi yanayofanya kazi na serikali ya DRC, PARECO-FF (Coalition des Patriotes Résistants Congolais-Force de Frappe), ikilishutumu kwa “kuendesha miradi haramu ya uchimbaji madini na ushuru huko Rubaya”.

Kundi hilo, linaloundwa zaidi na Wahutu kutoka DRC, lilidhibiti migodi katika eneo la Rubaya – ambayo ina madini ya thamani muhimu kwa sekta ya teknolojia, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi -kuanzia mwaka 2022 hadi mapema 2024, kulingana na Marekani.

John Hurley, Naibu Waziri wa fedha wa Marekani, alisema kuwa “madini ya migogoro yanaua raia wa Congo, kuchochea rushwa, na kukvuruga biashara halali za kuwekeza nchini DRC.”

“Wizara ya fedha haitasita kuchukua hatua dhidi ya mashirika ambayo yanainyima Marekani na marafiki zetu kupata madini ya thamani ambayo ni muhimu kwa usalama wa taifa letu,” alisema.