Na Munir Shemweta, WANMM

Baadhi ya wananchi katika halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya wameipa pongezi wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuandaa Klinik ya Maalum ya Ardhi kwa ajili ya kuongeza kasi ya umlikishaji ardhi katika maeneo yao.

Klinik Maalum ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mbarali imeanza tarehe 6 Agosti 2025 na inatarajiwa kumalizika tarehe 18 Agosti 2025 na inahusisha viwanja 30,700 vilivyopangwa na kupimwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP). Mradi huo ulifanyika katika Kata ya Rujewa, Ubaruku, Lugelele, Mabadaga, Igulusi, Kongoromswiswi na Madibira.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti tarehe 14 Agosti 2025 wakati wa Klinik Maalum ya ardhi ilinayofanyika kijiji cha Ubaruku wilayani Mbarali, wananchi hao wamesema uamuzi wa wizara ya ardhi kuandaa klinik hiyo ya ardhi umewarahisishia kupata hati milki za maeneo bila ya usumbufu.

Mmoja wa mwananchi aliyejitokeza kupata huduma (kulia) akihudumiwa na watumishi wa Wizara ya Ardhi wakati wa Klinik Maalum ya Ardhi katika kijiji cha Ubaruku wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya.

‘’Hili walilofanya wizara kuandaa klinik Maalum ya Ardhi katika eneo hili la Mbarali kwa kweli limetufurahisiha sana kwa kuwa tumepata hati hap hapa, tumesubiri kwa muda mrefu kupata hati na hatimaye kilio chetu kimesikilizwa’’ amesema Juma Omar mkazi wa Ubaruku.

Kwa mujibu wa wakazi hao wa Ubaruku, maeneo yao waliwekewa mawe kwa muda mrefu lakini umilikishaji haukufanyika kwa wakati jambo lililowafanya wananchi kuwa na mashaka juu ya zoezi la umilikishaji.

Wamesema kuwa, iwapo kasi ya umilikishaji inayofanyika hasa kwenye maeneo yaliyoainishwa basi wananchi wa maeneo husika wataweza kunufaika na umiliki wa ardhi yao kwa kupatiwa hati milki inayoweza kutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kukopea katika taasisi za fedha.

Sheikh Haroun Mkanyanga, mkazi wa Igawa mbali na kuipongeza wizara ya Ardhi kwa kuandaa Klinik Maalum amewataka wananchi wa Mbarali kuchangamkia zoezi hilo kwa kuwa limewarahisishia kazi ya kufuata huduma hiyo ya ardhi umbali mrefu.

Wananchi wakipata huduma wakati wa Klinik Maalum ya Ardhi inayoendelea katika Halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoa wa mbeya.

‘’Niwatake wamiliki wenzangu wa ardhi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hii ya ardhi hususan hati milki kwa kuwa ardhi ni kila kitu na unapokuwa na umiliki utaepukana na migogoro ya ardhi kama vile migogoro ya mipaka’’ amesema

Kwa upande wake Mratibu wa Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) Elia Kamihanda amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbarali kujitokeza kwa wingi kupata huduma kupitia zoezi hilo lililoanza tarehe 6 Agosti 2025 na kuhitimishwa tarehe 18 Agosti 2025 kwa kuwa huduma zimesogezwa karibu na wananchi

‘’Niwaombe ndugu zangu wa Mbarali kuchangamkia zoezi hili kwa kuwa limewasogeza huduma lakini mbali na hapa watalazimika kufuata huduma katika ofisi zetu jambo ninaloona halileti afya wakati huduma kwa sasa zipo hapa’’ amesema Kamihanda.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha Klinik Maalum ya Ardhi kwa ajili ya kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi kwenye maeneo ambayo mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki (LTIP) umetekelezwa.

Klinik hiyo maalum ya ardhi inafanyika Dar es Salaam katika manispaa ya Ilala, Dodoma eneo la Mpunguzi, Mbeya halmashauri ya Mbarali na mkoa wa Shinyanga katika halmashauri ya Kahama pamoja na Manispaa ya Shinyanga.

Mratibu wa Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) Elia Kamihanda akizungumza wakati wa ufunguzi wa Klinik Maalum ya Ardhi katika kijiji cha Ubaruku Mbarali Mbeya (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Kupitia klinik hiyo huduma mbalimbali zitatolewa kama vile umilikishaji ardhi wa papo kwa hapo kwa wamiliki waliokamilisha taratibu za umiliki, utoaji elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa utoaji huduma za ardhi kidigiti (e-Ardhi) na Usaidizi wa ufunguaji wa akaunti ya Mwananchi kwenye mfumo wa e-Ardhi.

Huduma nyingine ni Uhakiki na utambuzi wa viwanja vya Wananchi Uwandani, Utoaji wa namba ya malipo (control number) za ada mbalimbali za Serikali kwa ajili ya umilikishaji pamoja na Upokeaji, usikilizaji na utatuzi wa migogoro kiutawala.