Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani kimetoa rai kwa wagombea wa ubunge na udiwani walioongoza katika mchakato wa kura za maoni kuacha kufanya mbwembwe na kutengeneza makundi, na badala yake wawe watulivu kusubiri vikao vya juu vya ngazi ya maamuzi.

Aidha, chama hicho kimeonya kuwa kiongozi au mwanachama yeyote atakayekiuka maelekezo na miongozo hiyo atakuwa amejiondoa mwenyewe katika mchakato, kwani chama kina taratibu zake.

Akizungumza kuhusu yaliyojiri katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani Agosti 14,2025 ,Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo mkoani humo David Mramba, alieleza majina ya wagombea wa udiwani hayatatangazwa hadi Sekretariet ya Chama Taifa itakapotoa maamuzi rasmi.

“Mchakato wa kupata wagombea kupitia kura za maoni umemalizika salama, agost13  tumefanikisha kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa ambapo tumejadili majina ya wagombea wa ubunge na udiwani”

“Sasa tutasubiria vikao vya juu kufanya maamuzi ya mwisho kujua nani atapeperusha bendera ya chama katika uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza Mramba.

Aliongeza kuwa majina yote ya wagombea wa udiwani yanakwenda katika Sekretarieti ya CCM Taifa na yatarudishwa baadaye kwa hatua zaidi kwenye ngazi ya mkoa.

Kuhusu wagombea wa ubunge, Mramba alisema majina yao yanangoja vikao vya Sekretarieti ya Taifa, Kamati Kuu, na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa hatua za mwisho za kimaamuzi.

Pia, alisema Chama mkoa kinawataka wale walioongoza katika nafasi za Ubunge wa Viti Maalum kutotumia ushindi huo kujibweteka, bali waendelee kusaka kura za Urais .