Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega Mkoani hapa imewahukumu  watu 4 wakazi wa Mtaa wa Maporomoko kata ya Nzega Mashariki kutumikia kifungo cha miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kutumia silaha.

Akitoa hukumu hiyo jana Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya hiyo Saturin Mushi amesema kuwa ametoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine

Ametaja waliotiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo kuwa ni Adam Nkulu(22), Juma Ramadhani(20), Ramadhani Rugaraba(25) na Amosi Elias(23) ambapo wote kwa pamoja watatumikia kifungo cha miaka hiyo kwa kosa hilo.

Alieleza kuwa vijana hao wana nguvu za kufanya kazi na kujipatia kipato halali lakini wao waliamua kutumia njia mkato ya kufanya uhalifu ili kujipatia fedha.

Alibainisha kuwa kitendo cha kushambulia mwenzako kwa namna yoyote ile ikiwemo kutumia mapanga na kumsababishia maumivu na kupora mali yake hakikubaliki katika jamii yoyote ile, huo ni ujambazi.

Awali Wakili wa Serikali Enock Kigolya aliiambia mahakama hiyo kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Aprili 09 mwaka huu majira ya saa nne usiku katika eneo la Kashishi, Mtaa wa Maporomoko, Kata ya Nzega Mashariki wilayani hapa.

Alisema kuwa watuhumiwa walimvamia Amani Clement Mpitanjia na kumshambulia kwa kumkatakata mapanga na kumwibia kiasi cha 20,000/-alizokuwa nazo mfukoni, hivyo akaomba mahakama itoe adhabu kali.  

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, watuhumiwa hao waliomba mahakama hiyo kama itawatiwa hatiani iwapunguzie adhahabu kwa kuwa ni kosa lao la kwanza na bado ni wadogo na wanategemewa na wazazi wao.

Baada ya kuwatia hatiani kwa makosa hayo, mahakama ilitoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja ili iwe fundisho miongoni mwa na kwa vijana wengine wenye tabia kama hizo za uporaji.