Na Pendo Nguka, JakhuriMedia, Dar es Salaam

Aliyekuwa mbunge wa Kisesa na mwanasiasa mkongwe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luaga Mpina ambaye kwa sasa ni mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo ameeleza kuwa amekihama CCM kwa sababu kimeshindwa kabisa kutekeleza wajibu wake kwa wananchi na kimepoteza dira ya kuongoza nchi.

Mpina amesema kuwa licha ya kuzaliwa ndani ya familia ya CCM na kulelewa katika misingi ya chama hicho, ameamua kuchukua uamuzi mgumu wa kujiunga na chama cha upinzani kwa lengo la kusimamia maslahi ya wananchi na kulinda rasilimali za taifa.

“Mimi ni mwana CCM halisi, nimekulia ndani ya chama hicho lakini leo hii nimesimama mbele yenu kama mgombea kupitia ACT-Wazalendo.

“CCM hii imechoka, imepoteza dira na imeasi misingi ya waasisi wake kwa kushindwa kuzuia ufisadi badala yake imekuwa kinara wa kuuza rasilimali za taifa kana kwamba ni peremende mitaani,” amesema Mpina.

Katika hotuba yake, Mpina ameeleza kuwa ameona kabisa kuna kupuuzwa kwa hoja za msingi kutoka kwa wananchi huku viongozi wa sasa wakijaribu kuhalalisha kila jambo, hata kama ni kifo cha mtu, kwa kauli zisizo na huruma wala uwajibikaji.

Akizungumzia masuala ya kiusalama Mpina ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha kuwa watu wasiojulikana wanajulikana na wote wanaohusika na vitendo vya utekaji na mauaji wanafikishwa mbele ya sheria.

“Ni lazima tuwape wananchi majibu. Watu wasiojulikana ni nani na katika Serikali yangu, watu hawa watajulikana na watachukuliwa hatua bila haya wala uoga,” amesisitiza.

Mpina aliendelea kueleza kuwa CCM ya sasa siyo tena chama kilichorithi misingi ya waasisi kama Mwalimu Julius Nyerere bali ni chama kilichoteleza kutoka kwenye maadili misimamo ya kizalendo na sasa kimekuwa kikihujumu ajenda za maendeleo za wananchi.

“Chama hiki hakina tena mwelekeo na kama lingekuwa gari basi leo hii lingepaswa kupimwa kama chuma chakavu na cha kusikitisha ni kwamba walio ndani ya chama hicho hawana uchungu wala hawashtushwi na kinachoendelea,” aliongeza.

Pia ameeleza kuwa kumekuwa na vikao vya siri ndani ya CCM ambavyo vinaendeshwa kwa misingi ya upendeleo na kama kuna mwanachama akionekana kuwa na msimamo au mtazamo tofauti, jina lake linakatwa au anapokonywa nafasi ya uongozi bila maelezo ya kina.

Aidha Mpina ameweka wazi dhamira yake ya kuleta mabadiliko kupitia ACT-Wazalendo huku akiahidi kushirikiana na wananchi kuandika historia mpya ya Tanzania yenye haki, usawa na maendeleo ya kweli kwa wote.