Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Baada ya kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika jana jijini Dodoma, Chama cha NCCR Mageuzi leo Agosti 15,2025 kinatarajiwa kuelekea Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuchukua fomu za uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za juu kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kikao hicho kilichofanyika jana Agosti 14, kiliweka ajenda ya uchaguzi kuwa kipaumbele kikuu na kufikia maamuzi ya mwisho kuhusu wagombea wake.
Balozi Dkt. Evaline Wilbard Munisi aliteuliwa kwa kura zote 58 kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiungana na Haji Ambar Khamis ambaye uteuzi wake kama mgombea urais wa Jamhuri ulithibitishwa siku chache zilizopita.

Aidha, Leila Rajabu Khamis aliteuliwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 57 kati ya 58 za wajumbe waliohudhuria kikao hicho.
Pamoja na uteuzi huo, NCCR Mageuzi pia iliidhinisha Ilani ya Uchaguzi 2025/2030 yenye vipaumbele 11, ikiwemo sekta ya afya, usawa wa kijinsia na makundi maalum, mifugo, madini, maliasili na utalii, usalama wa taifa na kurejesha maadili ya kitaifa. Kipaumbele cha maadili na uadilifu kimepewa msisitizo wa kipekee.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti Taifa wa Chama cha NCCR -Mageuzi Haji Ambar Khamis,uteuzi wa wagombea hao umefanyika kwa makubaliano ya pamoja na kuakisi dira ya chama inayolenga maendeleo ya watu na siyo kushindana kwa dhana ya kuiondoa CCM pekee.
“Niwatoe hofu ndugu zangu, kama tulivyosema kwenye azimio letu, lazima tushinde,” amesema mmoja wa viongozi, akibainisha kuwa chama kimesimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote 162, na hakitegemei ruzuku bali michango ya wananchi wake.

Kwa upande wake, Bw. Sisty Nyahoza, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa aliyemwakilisha Msajili wa Vyama, aliipongeza NCCR Mageuzi kwa kufanikisha kikao chake cha kikatiba kwa utulivu na kuzingatia misingi ya demokrasia.
Amewataka viongozi na wanachama kuendesha kampeni kwa kuzingatia sheria na katiba kuelekea kuanza kwa kampeni rasmi Agosti 28, 2025.