Na Mwandishi Wetu, Simiyu

Chama cha ACT Wazalendo kimefanya mapokezi rasmi ya mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Luhaga Mpina, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Kisesa, Mkoa wa Simiyu.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mgombea Mwenza wa Urais wa Tanzania, Fatma Fereji, pamoja na Mgombea Urais wa Zanzibar, Othman Masoud. Aidha, viongozi mbalimbali wa chama hicho walihudhuria akiwemo Kiongozi wa Chama (KC) Semu Dorothy, aliyesimamia mapokezi hayo.

Katika tukio hilo, Mgombea Urais Mpina na Mgombea Mwenza wake walionesha hadharani begi la fomu za kuomba kugombea Urais wa Tanzania, hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Vilevile, Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Mhe. Zitto Kabwe, alimtambulisha rasmi Mpina kwa wakazi wa Jimbo la Kisesa, akisisitiza mshikamanio wa chama hicho katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, KC Dorothy alihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanailinda kura yao wakati wa uchaguzi, akisema kaulimbiu ya chama ni #LindaKura na #MuhuniHasusiwi.