Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa SELF Microfinance, Santieli Yona amesema huduma za kifedha bado ni eneo linalohitaji kuwekewa mkazo hasa katika kutoa elimu kwa jamii.

Amesema kuwa mfuko wa SELF Microfinance ni mfuko uliyo chini ya Wizara ya Fedha na inayojihusisha na utoaji wa mikopo kwa vikundi, taasisi mbalimbali na mtu mmoja mmoja kwa riba nafuu.

“SELL Microfinance imekuwa ikitoa elimu ya fedha mara kwa mara kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo maonesho ya Nanenane, Sabasaba, makongamano na kupitia vyombo vya habari ilinkuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata elimu ya fedha, kwa kuwa bado wengi hawana uelewa wa matumizi ya mikopo” amesema.

Akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri (TEF) na taasisi hiyo, kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square, jijini Dar es Salaam leo Agosti15, 2025, amesema kuwa kama wananchi watapata elimu sahihi juu ya matumizi sahihi ya mikopo itasaidia kulipika bila ya vikwazo.

” Wengi hawana uelewa wa matumizi ya fedha za mikopo, huwezi kuja kuomba mkopo bila ya kujiandaa ya namna ya kurejesha na hapa ndipo wengi wanaposhindwa na kusababishwa kukwama kurejesha fedha za mikopo na kuingia kwenye migogoro.

“Ni vizuri kabla ya kukopa ufanye tathmini ya kina kuhusu utumizi wa fedha hizo kwenye biashara yako. Ukijipanga vizuri, utakuwa na uhuru na kujiamini. Lakini ukishindwa kurejesha, inaleta changamoto kwa wakopeshaji na inaweza kuongeza gharama za mikopo.

” SELL Microfinance inatoa mikopo kwa kuzingatia hilo ili kuepuka mkopaji kuingia kwenye changamoto ya kushindwa kurejesha ni vyema kwanza kabla ya kutoa mkopo muhusika apate elimu” amesema.

Amesema kuwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa SELF Microfinance imeweza kuwajengea uwezo taasisi 549 kwa kutoa ushauri mbalimbali, kukaa nazo na kuzisaidia namna ya kujiendesha.

Bi. Yona amesema kuwa moja ya mafanikio waliyoyapata ni kutengeneza ajira. “Sisi tunatoa mikopo kwa taasisi zinazokopesha na pia kwa wajasiriamali. Wajasiriamali hawa wanapopewa fedha, wanajiajiri na kutoa fursa kwa watu wengine,” amesema.

Ameeleza kuwa katika kipindi hiki, wameweza kutoa ajira zipatazo 183,000, jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa taifa, kwani si Serikali pekee inayoweza kutoa ajira, bali kila mmoja anaweza kujiajiri na kujikimu.

Mafanikio mengine ni kuanza kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni utekelezaji wa ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan. Amesema mikopo hiyo itakapowafikia wananchi, itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira.

Bi. Yona ameongeza kuwa, wanapenda kufuatilia kuona kama huduma zao zinabadilisha maisha ya wanufaika. “Kila baada ya muda tunapenda kujua walikuwa wapi, mikopo imewasaidiaje, na wapo wapi sasa,” amesema.

Amefafanua kuwa mkopo unapotumiwa vizuri unaweza kukuza biashara, lakini usipotumiwa ipasavyo unaweza kusababisha matatizo.

“Unapotumia mkopo vizuri, uwe na uhakika utakusaidia. Lakini ukitumia kinyume na malengo, au bila usimamizi mzuri, fedha hazitakusaidia na zinaweza kukuingiza kwenye matatizo zaidi,” alisema.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto, ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kukosa elimu ya fedha, kushindwa kufanya tathmini kabla ya kukopa, na hulka ya watu wachache kutojali kurejesha mikopo.