Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa hatua ya Urusi kukataa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano inatatiza juhudi za kumaliza vita.

“Tunaona kwamba Urusi inakataa wito wa kusitishwa kwa mapigano na bado haijaamua ni lini itakomesha mauaji. Hii inafanya hali kuwa ngumu,” alisema katika taarifa yake katika mtandao wa X.

Siku ya Jumatatu, kiongozi huyo wa Ukraine ataelekea Washington DC, ambapo Rais wa Marekani Donald Trump amesema atamhimiza Zelensky kufikia makubaliano ya amani.

Trump amesema anataka kuachana na usitishaji vita nchini Ukraine ili kuelekea moja kwa moja kwenye mkataba wa amani ya kudumu baada ya mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Katika mabadiliko makubwa ya msimamo wake, rais wa Marekani alisema katika mtandao wa Truth Social kufuatia mkutano wa kilele wa Ijumaa huko Alaska, kwamba hii itakuwa “njia bora ya kumaliza vita vya kutisha kati ya Urusi na Ukraine”, akiongeza kwamba mara nyingi usitishaji mapigano “huwa haudumu”.

Kufuatia mazungumzo ya simu na Trump baada ya mkutano huo, Zelensky alitoa wito wa kuwepo kwa amani ya kweli na ya kudumu, huku akiongeza kuwa “mashambulizi ya risasi” na mauaji lazima yakome.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii Zelensky alielezea mahitaji yake ya “amani endelevu na ya kudumu” na Moscow, ikiwa ni pamoja na “dhamana ya kuaminika ya usalama” na kurudishwa kwa watoto ambao anasema “walitekwa nyara kutoka maeneo yanayokaliwa” na Urusi.