Na Haji Mtumwa, JamhuriMedia, Zanzibar

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, huku ikisisitizaa kura ya mapemaa ipo kama kawaida.

Tangazo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji George Joseph Kazi, katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Makao Makuu ya ZEC, Maisara, Mjini unguja.

Akitoa taarifa hiyo muhimu, Jaji Kazi alisema kuwa mchakato mzima wa uchaguzi sasa unaingia katika hatua za utekelezaji, huku ZEC ikiwa tayari kuweka mazingira bora, salama na ya haki kwa kila mpiga kura.

“Kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, ZEC ina mamlaka ya kutangaza tarehe ya uchaguzi. Tunawaarifu kuwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafanyika Oktoba 29, 2025,” alisema Jaji Kazi.

Jaji Kazi alieleza kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea kwa nafasi za Urais, Uwakilishi na Udiwani utaanza rasmi Agosti 28 hadi Septemba 10, 2025, saa 10:00 jioni na Siku ya uteuzi wa wagombea imepangwa kufanyika Septemba 11, saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Kampeni za uchaguzi zitaanza mara baada ya uteuzi wa wagombea mnamo Septemba 11 saa 10:01 jioni, na zitakamilika Oktoba 27 saa 12:00 jioni.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alitangaza kuwa kwa mara nyingine ZEC itatekeleza upigaji kura ya mapema, utakaofanyika Jumanne, Oktoba 28, 2025 – siku moja kabla ya uchaguzi mkuu.

“Kura ya mapema ni kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha Sheria ya Uchaguzi, na itawahusisha watendaji wote watakaokuwa na majukumu ya kiuchaguzi siku ya uchaguzi,” alisema.

Watendaji hao ni pamoja na wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wao, wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, askari polisi waliopangwa kwenye vituo vya uchaguzi, wajumbe wa ZEC, na watendaji wa Tume wanaohusika moja kwa moja na mchakato wa uchaguzi.

Jaji Kazi pia alieleza kuwa ZEC imejipanga kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye ulemavu wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kuweka vifaa saidizi katika vituo vya kupigia kura.

“Tume itahakikisha kundi hilo lianatumia haki yao ya kupiga kura kwa heshima na kwa uhuru kama ilivyo kwa wananchi wengine wote,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo aliwataka wadau wote wa uchaguzi wakiwemo vyama vya siasa, wagombea, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Tume kuhakikisha uchaguzi wa unafanyika kwa amani na utulivu.

“Tunawaomba wadau wote kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa na Tume. Vyama vya siasa na wagombea waepuke lugha za uchochezi na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani,” alisema.

Vilevile, aliwataka waandishi wa habari kuzingatia maadili na weledi wanaporipoti habari za uchaguzi ili kutoa taarifa sahihi na zisizopotosha umma.

“Vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha jamii. Tume inatarajia waandishi watatekeleza wajibu wao kwa uadilifu ili kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa amani, kama inavyoelekezwa na kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu 2025,” aliongeza.

Jaji Kazi aliwapongeza wananchi kwa kushiriki katika hatua zote za maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo uandikishaji wa wapiga kura, uhakiki wa orodha ya wapiga kura na ugawaji wa vitambulisho.

“Tume imepokea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi. Tunaomba waendelee kushiriki katika hatua zote za uchaguzi hadi mchakato mzima utakapotamatika,” alihitimisha.

Kwa mujibu wa ZEC, kuhesabu kura na kutangaza matokeo kutaanza mara moja baada ya upigaji kura kukamilika, kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 1, 2025.