Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WorldVeg) iliyopo Tengeru mkoani Arusha, imesema itahakikisha kilimo kinakuwa na tija kubwa zaidi kwa wakulima wa Tanzania na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika kwa kuendeleza tafiti za kina juu ya mbegu bora pamoja na kuzalisha wataalamu wengi zaidi watakaowafikia wakulima kirahisii.
Akizungumza katika mafunzo ya siku tatu juu ya uhifadhi wa mbegu yaliyomalizika katika kituo hicho, Mkurugenzi Mkazi wa WorldVeg, Bi. Colleta Ndunguru, amesema kuwa taasisi hiyo imejikita katika kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wazalishaji na watafiti wa ndani na kimataifa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kitaifa kama Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), Kituo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea (NPGRC), na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

“Msingi wa kilimo bora ni upatikanaji wa mbegu bora za kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti wa kisayansi wa kina ili kuhakikisha mavuno bora na kilimo chenye tija kwa mkulima,” alisema Bi. Colleta.
Alibainisha kuwa taasisi hiyo imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kisasa ikiwemo maabara na benki ya vinasaba ya mbegu ambazo hukusanywa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya utafiti wa kina.
Katika kipindi cha wiki mbili , WorldVeg iliendesha awamu mbili za mafunzo maalumu juu ya mbinu bora za ukusanyaji, uhifadhi, na uhuishaji wa mbegu, ambapo wataalamu kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), TPHPA na TARI walihudhuria.
Mafunzo hayo yalifundishwa na wataalamu kutoka makao makuu ya taasisi hiyo nchini Taiwan pamoja na wale waliopo hapa nchini.

“Tumeingia mikataba ya ushirikiano na taasisi mbalimbali kwa lengo la kukuza sekta ya kilimo nchini kwa kuzalisha wataalamu zaidi na kufanya tafiti endelevu za mbegu bora,” aliongeza Bi. Colleta.
Amesema kuwa taasisi hizo pia kwa pamoja zimekuwa zikiwafikia wakulima moja kwa moja kwa ajili ya kutoa elimu ya kitaalamu, kufanya ukaguzi wa mbegu, na kuwashauri kuhusu mbinu bora za uzalishaji.
“Tunajivunia ushirikiano huu na mafunzo haya ya mara kwa mara ambayo ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya kilimo chetu,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha kuwa wataalamu waliopatiwa mafunzo wanawafikia wakulima vijijini na kuwahamasisha kuhusu mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, kuanzia kwenye utambuzi wa mbegu bora – ikiwemo za asili – maandalizi ya mashamba, hadi upatikanaji wa masoko kwa mazao, hasa mbogamboga.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Pavithravani Venkataramana kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa ya manufaa makubwa kwao, kwani yamewapa fursa ya kujifunza kwa nadharia na vitendo namna bora ya kuandaa na kuhifadhi mbegu.
“Kilimo cha kisasa kinahitaji utafiti wa kina, siyo tena kilimo cha mazoea. Tunahitaji mbegu bora na maarifa sahihi ili kuwa na uhakika wa mavuno ya kutosha,” alisema.

Kwa upande wake, Mtafiti kutoka TARI, Bw. Emmanuel Katamba, alisisitiza umuhimu wa kuwajengea wakulima uwezo wa kutambua mbegu bora kwa urahisi na kutumia mbegu hizo kwa usahihi.
Naye Bw. Abdul Shango, Mtaalamu wa Mbegu kutoka WorldVeg-Arusha , alieleza kuwa taasisi hiyo imefanya tafiti mbalimbali juu ya mbegu zinazotumika katika nchi mbalimbali za Afrika, ambazo zimeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa na mabadiliko ya tabianchi.
“Utafiti wetu umeonyesha kuwa mbegu zinazofanyiwa utafiti kwa kina si tu huongeza tija ya mazao bali pia zinasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za mazingira na tabianchi,” alieleza Bw. Shango.
