Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imetenga Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), hatua inayolenga kuongeza wataalamu na kuboresha teknolojia katika sekta ya uchukuzi nchini.
Akizungumza leo Agosti 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Usafirishaji, Logistiki na Usimamizi, sambamba na kuzindua sherehe za miaka 50 ya kuanzishwa kwa NIT, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakuwa ya kisasa, salama na yenye ushindani wa kimataifa.
“Leo tunaanzisha kituo kikubwa cha umahiri ambapo Rais Samia amepeleka Sh Bilioni 50 kwa ajili ya kuanzishwa kwake. Tafiti zinazofanyika NIT zikitekelezwa kwa vitendo zitasaidia kutatua changamoto nyingi katika sekta ya uchukuzi. Haitakuwa na maana kama tuna miundombinu ya kisasa bila wataalamu, ndiyo maana Serikali inaendelea kuwekeza kwenye vyuo vya sekta hii,” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, amesema sekta ya usafirishaji ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, na juhudi za Serikali kupitia miradi mikubwa ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) zimeanza kuonyesha matokeo ya moja kwa moja.
“Rais Samia ameweka kipaumbele kikubwa kwenye sekta hii na kielelezo kikubwa ni SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Hapo zamani tulitumia saa tisa kwa basi, leo tunatumia masaa matatu pekee kwa treni,” amrongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema chuo hicho kimekua kutoka wanafunzi 78 mwaka 1975 hadi zaidi ya wanafunzi 17,000 wa kozi ndefu na zaidi ya 10,000 wa kozi fupi kila mwaka, huku kikiwa na ithibati inayotambulika na Umoja wa Ulaya na TCAA.
“Sasa tuna vifaa vya kisasa na wahitimu wetu wanakubalika kimataifa. Moja ya hatua kubwa tunazochukua ni kufungua kampasi mpya KIA kwa ajili ya mafunzo ya marubani na Lindi kwa ajili ya wataalamu wa usafiri wa majini,” amesema.
Naye Meneja wa Kampuni Tanzu ya NIT, Dkt. John Mahona, amesema kampuni hiyo itashirikiana na walimu katika ubunifu wa kiteknolojia ili Watanzania waweze kutengeneza magari na mitambo ya kisasa kwa manufaa ya taifa.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni: “Kutumia Mifumo Bunifu na Endelevu kwa ajili ya Kuimarisha Sekta ya Usafiri na Usalama.”