Na Cresensia Kapinga, JamhuriMesia, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limewatia mbaroni watu saba kwa tuhuma za kupatikana wakiwa na nyara za serikali, meno ya Tembo 64, kati yake mazima yakiwa 8 na vipande 56,meno ya Kiboko 145 na meno ya Ngiri mawili yenye thamani ya sh. Milioni 314 684,419.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 21, 2025 ofisini kwake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya amesema kuwa watuhumiwa hao saba majina yao yameifadhiwa kwa upelelezi zaidi ambapo watuhumiwa hao walikutwa na nyara za Serikali zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko ya Sandarus yakiwa yamefichwa kichakani na mengine kuyafukia ndani ya shimo walilokuwa wamechimba kisha kuweka nyasi kavu kitendo ambacho ni kinyume Cha Sheria.

Alifafanuwa kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 18, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgazini Wilaya ya Songea na Masigira iliyopo kata ya shule ya Tanga Manispaa ya Songea ambapo katika mwendelezo wa msako na oparesheni zinaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la hifadhi la wanyama pori ( TAWA) kwa kuwasaka wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali pamoja na uwindaji haramu mkoani Ruvuma na kwamba watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara tu baada ya kukamilisha upelelezi.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani humo Agosti 15, mwaka huu Majira ya saa 11 alfajiri huko katika maeneo ya Mjimwema Halmashauri ya Manispaa ya Songea walifanikiwa kumkamata Michael Lusekelo Mwakifuna ( 50) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Mjimwema akiwa na bidhaa bandia zilizotengenezwa ambazo ni pombe aina ya Mastar Potable spirit chupa 09,pombe aina ya Konyagi 750 ml chupa 07, chupa 02 za konyagi 200ml, Smart gin 200ml chupa 03 zilizotengenezwa bila leseni.

Kamanda Chilya amesema kuwa mtuhumiwa huyo pia alikutwa na vifaa vya kutengenezea pombe hizo haramu alivyokuwa akivitumia kutengenezea pombe ambazo ni kemikali ikiwa kwenye chupa ndogo mbili zikiwa na label PN, sticker za TRA 06, Soltape Moja kubwa,Kimiminika kwenye Jaba la rangi ya kijani mpauko,vizibo kwenye mfuko wa sanadarusi,kamba za manila bunda 13,madumu tupu 38, boksi la chupa za JB kubwa na ndogo,mifuko miwili ya chupa tupu za Smart gin,mifuko 05 ya Sandarusi ikiwa na chupa tupu za konyagi,mfuko mmoja wa Sandarusi ukiwa na maboksi yenye nembo za Smart gin pamoja na mfuko mmoja wa Sandarusi wenye maboksi yenye nembo za konyagi na vizibo vyake vikiwa ndani ya boksi.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Chilya amesema kuwa mtuhumiwa alikuwa akitengeneza bidhaa hizo bandia ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga huko eneo la Mjimwema Manispaa ya Songea na upelelezi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kwa lengo la kubaini mtandao wa watu wanaojihusisha na kutengeneza pombe bandia na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.