Na Cresencia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Moria maarufu kwa jina la Mama Yusta baada ya kumjeruhi Kanisia Hinju (30) mkazi wa kijiji cha Kihuru wilayani Nyasa kwa kumng’ata meno kwenye mdomo wa chini mpaka kumnyofoa kipande kisha kukimbia nacho kusikojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 21, 2025 ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya amesema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 13, mwaka huu, Majira ya saa 10 jioni katika Kijiji cha Kihuru kilichopo kata ya Lituhi wilayani Nyasa na kwamba chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokea baina ya majeruhi na mtuhumiwa huyo baada ya mtoto wa majeruhi kupigwa na mtuhumiwa kitendo kilichosababisha mama wa mtoto ambaye ni Kanisia Hinju kushindwa kuvumilia na kuibuka ugomvi huo.

Ameeleza kuwa juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea na majeruhi amelazwa katika Hospitali ya St. Elizabeth iliyopo Lituhi kwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.