Mkuu wa Kitengo cha kushughulikia Makosa dhidi ya Binadamu, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Stella Mtabihirwa leo Agosti 22, 2025 amefunga mafunzo ya uwekaji alama silaha na utunzaji wa taarifa kwa Askari Polisi Jijini Dodoma, Mafunzo ambayo yalikuwa yakiendeshwa na RECSA.
Akifunga mafunzo hayo baada ya kuwatunuku vyeti vya ushiriki, DCP Stella amewataka kutumia vyema utaalamu walioupata katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema zoezi la kuweka alama silaha na kutunza taarifa za silaha ni muhimu ili kudhibiti silaha zisiingie katika mikono ya wahalifu na pale zinapotumika katika uhalifu ziweze kutambulika kwa haraka na kurahisisha upelelezi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Mtendaji wa RECSA na Mkufunzi wa Mafunzo hayo Eric Kayiranga amesema zoezi la kudhibiti silaha ndogondogo na nyepesi katika nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika ni utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Nairobi.
Amesema RECSA itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Jeshi la Polisi katika kutoa mafunzo na vifaa kama walivyofanya ambapo wametoa mashine mpya za kisasa mbili kwa ajili ya zoezi la uwekaji alama silaha.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti na Usajili wa Silaha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amesema washiriki wa mafunzo hayo watakuwa Walimu wa Walimu (TOT) ili kuwafikia Askari wengine ambao bado hawajapata mafunzo.


