Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
VIONGOZI wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) wamekutana na Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, pamoja na Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, kujadili changamoto zinazowakabili wanahabari nchini, hususan mikataba ya ajira na mazingira bora ya kazi.
Kikao hicho kilifanyika Agosti 21, mwaka huu 2025 jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri na kuhudhuriwa pia na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Ridhiwani amesema wizara yake haitaridhika kuona wanahabari wengi wakifanya kazi katika mazingira duni na bila mikataba ya ajira.
“Nimewaita hapa tuzungumze kuhusu changamoto zinazowakabili. Mimi binafsi nazifahamu na tunataka kuzitafutia suluhisho. Hali hii haiwezi kuendelea,” amesema.
Amesema ni lazima kila sekta nchini ifuate sheria za kazi zilizopo na kuonya tabia ya baadhi ya waajiri kuendesha mambo kwa ‘ujanja ujanja’, hali inayowaathiri wafanyakazi wanapostaafu au wanapopatwa na matatizo.
“Tulizungumza Arusha, na tukakubaliana tukutane tena. Leo tupo hapa na Kamishna wa Kazi ili tujadiliane namna ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wanahabari,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, ameomba msaada wa Serikali kupitia Wizara hiyo kuhakikisha waajiri katika sekta ya habari wanazingatia sheria za kazi kama ilivyo kwa sekta nyingine.
“Zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari hawana mikataba ya ajira, hawana bima ya afya, wala uanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Wengine wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 katika hali hii,” amesema.
Ameomba wizara kupitia kwa Kamishna wa Kazi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyombo vya habari ili kuhakikisha waajiri wanazingatia sheria za kazi.
Akijibu hoja hizo, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na JOWUTA kutatua changamoto hizo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa wanahabari nao wanapaswa kufahamu haki zao na kuhakikisha wanafanya kazi chini ya mikataba halali.

“Tunaweza kufanya ukaguzi, lakini sekta hii ina changamoto za kimfumo, kama vile uwepo wa wanahabari wa kujitegemea (correspondents), wa mkataba wa muda (retainers), na baadhi yao kutokuwa na mikataba kabisa,” amesema.
Ameongeza kuwa wakati wa ukaguzi, waajiri hutoa mikataba ya walioajiriwa rasmi pekee, hivyo ni vigumu kubaini makundi mengine yasiyo rasmi kama taarifa sahihi hazitolewi.
“JOWUTA mnaweza kusaidia kwa kutoa taarifa za kweli kuhusu hali ya wafanyakazi katika kila chombo cha habari ili tuweze kuchukua hatua stahiki,” amesema..
Kamishna huyo pia aliahidi kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria za kazi kwa wanahabari ili wajue haki zao na wajibu wao.
Awali, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya, ameishukuru serikali kupitia Bodi ya Ithibati kwa kuhakikisha wanahabari wanakuwa na sifa stahiki za kitaaluma. Hata hivyo, aliomba jitihada hizo ziende sambamba na kuboresha maslahi ya wanahabari.

“Ni muhimu sana pamoja na kuhimiza Ithibati, Serikali ihakikishe wanahabari wanapewa mikataba, bima za afya, na haki nyingine za msingi,” amesema.
Viongozi wengine wa JOWUTA walioshiriki kikao hicho ni Mweka Hazina wa chama hicho, Lucy Ngowi ambaye ameelezea changamoto zinazowakabili wanahabari, ikiwemo kuachishwa kazi bila kufuata sheria, jambo linalochangia kukatisha tamaa na kuathiri utendaji wao wa kazi.