Na Ashrack Miraji, JamhuriMedia, Same
Watu wasiojulikana wamemshambulia kwa mapanga aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bw. Yusto Mapande, usiku wa Agosti 21, 2025 majira ya saa tatu usiku, wakati akiingia nyumbani kwake. Katika tukio hilo, Mapande alijeruhiwa mkononi na mguuni wakati akijitetea dhidi ya washambuliaji hao.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani vikali kitendo hicho, akieleza kuwa tayari Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kuwapata wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

“Nimesikitishwa sana na tukio hili. Tayari Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria. Serikali ipo kazini na haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuhusika,” alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wa Wilaya ya Same kuendelea kuchukua tahadhari wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku, kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi, na kuhakikisha wanarejea majumbani mapema endapo hakuna ulazima wa kuchelewa.
Kwa upande wake, Yusto Mapande, akizungumza jana jioni baada ya kutembelewa na Mkuu wa Wilaya nyumbani kwake kwa ajili ya kumjulia hali, alieleza kuwa watu waliomvamia walimfuata kwa kutumia pikipiki wakati akikaribia nyumbani huku akidhani ni wageni wenye nia njema.

Alieleza kuwa, alipokuwa akisubiri kufunguliwa kwa mlango (geti) ghafla vijana hao walimvamia na kuanza kumshambulia kwa mapanga na kuondoka na fedha kiasi cha shilingi milioni 20 alizokuwa nazo baada ya kutoka kwenye biashara zake.
Mapande alisema baada ya kushambuliwa alianza kuvuja damu nyingi na mwili wake kuanza kutetemeka, lakini kwa juhudi kubwa za madaktari wa Hospitali ya Mji Same, aliweza kuokolewa na anaendelea vizuri.
Aliongeza kuwa “mazungumzo ya vijana hao baada ya kunishambulia ikabidi nitege mkono karibu na shingo sasa zile damu zilizokuwa zinavija mkononi wakajua wamekata shingo na wameshaniua, nikajifanya nimezimia hapo nikasikia maneno yao na yalionesha wazi kuwa walitumwa na mtu kwa lengo baya.
