Dar es Salaam, Agosti 24, 2025 – Mwanaharakati na kada wa ACT-Wazalendo, Queen Julieth William Lugembe, leo amechukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Queen Julieth amesema hatua yake ni sehemu ya dhamira ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu.

“Ubungo ni miongoni mwa majimbo yenye changamoto nyingi lakini pia lina fursa kubwa za maendeleo. Nimeamua kusimama kugombea ubunge ili kushirikiana na wananchi kutatua changamoto hizo na kuibua fursa kwa manufaa ya wote,” alisema Queen Julieth.

Uchukuaji wa fomu hizo ni mwendelezo wa mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge unaoendelea nchi nzima kuanzia Agosti 14 hadi 27, chini ya usimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Queen Julieth atakabiliana na wagombea wengine kutoka vyama tofauti vya siasa, ambapo Jimbo la Ubungo limekuwa likihesabiwa kama moja ya maeneo yenye ushindani mkubwa kisiasa katika Jiji la Dar es Salaam.

ACT-Wazalendo kupitia kwa wagombea wake imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia maadili ya uongozi, utawala bora na maendeleo jumuishi kwa wananchi.