

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kuwaandaa vijana wengi zaidi wa Zanzibar kuwa wataalamu wa elimu ya anga.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na wanafunzi watano waliochaguliwa kutembelea makao makuu ya NASA yaliyopo Washington D.C., Marekani, pamoja na kushiriki katika mashindano ya NASA International Space Apps Challenge 2025 yatakayofanyika jijini Ibra, Oman. Mkutano huo umefanyika Ikulu Zanzibar leo tarehe 25 Agosti 2025.
Fursa hiyo imetokana na uwezo mkubwa waliouonesha waliposhiriki katika programu ya Kimataifa ya IASC (International Astronomical Search Collaboration) inayohusu uvumbuzi wa asteroids kwa kushirikiana na NASA (National Aeronautics and Space Administration) ya Marekani. Jumla ya wanafunzi 22 kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait ambao walishiriki kwa utambulisho wa Zanzibar Space Team na kufanikiwa kugundua asteroids mpya kupitia picha za anga zinazotumwa na NASA kwa programu ya Astrometrica.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdulla Said, amewataja Majid Khalfan Omar, Nadhifa Mashaka na Is-haka Harith Salim kuwa watatembelea makao makuu ya NASA nchini Marekani, huku Mulhat Abdallah na Feisal Issa Minchoum wanatarajiwa kuhudhuria Hackathon nchini Oman.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Royal Astronomy and Space Society, Bi. Amina Ahmad, amesema wanakusudia kuanzisha utalii wa anga Zanzibar pamoja na kuzindua programu maalum za mafunzo kwa wanafunzi kutoka skuli mbalimbali ili kujifunza taaluma hiyo.
Zoezi zima limeratibiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kushirikiana na asasi ya kiraia ya Royal Astronomy and Space Society pamoja na Eng. Abdulwahab Al Busaidi kutoka Oman Astronomical and Space Society.
Katika ziara hiyo inayotarajiwa kuanza Oktoba 2025, wanafunzi watapewa mafunzo kuhusu sayansi ya anga, uvumbuzi na teknolojia mbalimbali zitakazowawezesha kuimarika kitaalamu na kitaaluma.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amewakabidhi wanafunzi hao vyeti vyao vya kuhitimu.



