Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wiki hii kinaanza kishindo cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Agosti 28, 2025 zinaanza rasmi kampeni kwa ajili ya wagombea urais, ubunge na madiwani.
Kuna vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa nchini. Vyama 18 vimesimamisha wagombea urais. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshikilia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi.
Sitanii, vyama vilivyochukua fomu, ambavyo hapa ninataja mgombea urais kwanza na mgombea mwenza ni: 1. CCM – Dk. Samia Suluhu Hassan na Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi. 2. NRA – Hassan Almas na Hamis Hassan Majukumu. 3. AAFP – Kunje Ngombale Mwiru na Chumu Abdalla Juma. 4. MAKINI – Coaster Kibonde na Azza Haji Suleiman.
Vyama vingine ni 5. NLD – Doyo Hassan Doyo na Chausiku Khatib Mohamed. 6. UPDP – Twalib Ibrahim Kadege na Abdalla Mohamed Khamis. 7. ADA TADEA – Geoges Gabriel Bussungu na Ali Makame Issa. 8. UMD – Mwajuma Noty Mirambo na Mashavu Alawi Haji. 9. TLP – Yustas Mbatina Rwamugira na Amana Suleiman Mzee. 10. CCK – David Daud Mwaijojele na Masoud Ali Abdalla.

Wapo pia 11. CHAUMMA – Salumu Mwalimu na Devotha Minja. 12. DP – Abdul Mluya na Sadoun Abrahman Khatib. 13. SAU – Majalio Paul Kyara na Satia Mussa Bebwa. 14. CUF – Gombo Samandito Gombo na Husna Mohamed Abdalla. 15. ADC – Wilson Elias Mulumbe na Shoka Khatib Juma. 16. UDP – Salum Hussein Rashid na Juma Hamis Faki. 17. NCCR-Mageuzi – Haji Ambari Khamis and Dk. Eveline Wilbard Munisi. 18. ACT – Wazalendo – Luhaga Joelson Mpina na Fatma Abdulhabib Fereji.
Wagombea hawa wanasubiri uteuzi wasipowekewa pingamizi kufikia kesho saa 10 jioni. Tujiandae kusikiliza sera za wagombea hawa. Baadhi tumewasikia mara tu walipochukua fomu wameahidi kuzuia vitanda vya 6 x 6. Wengine wamesema watatoa leseni za vileo kwa kila mnywaji. Wapo walioahidi kuimarisha miundombinu ya barabara, maji, afya, umeme na huduma za jamii kwa kuongeza nidhamu ya watumishi wa umma.

Sitanii, jambo moja niliseme katika mchakato wa kupata wagombea urais katika vyama hivi 18 sijasikia tuhuma za rushwa kwa wagombea hawa. Inaonekana kiti cha urais bado kiko salama. Kelele nyingi nimezisikia kwenye kura za maoni za ubunge na udiwani.
Wagombea walioteuliwa na walioachwa na vyama vyao, ni malalamiko kila kona. Wengi wanasema rushwa imewaweka kando baadhi ya wagombea wazuri na kupitisha maboya katika vyama hivi.
Kwa hakika katika orodha iliyotangazwa kuna mikoa ambayo ninaona harufu za baadhi ya wagombea wa chama tawala kupururwa na wapinzani. Kuna majimbo matatu Dar es Salaam, inawapasa wateule kujiandaa kisaikolojia. Mkoa wa Kigoma nako kuna majimbo mawili, kabla waamini hawajatoa sadaka makanisani, biashara itakuwa imekwisha.
Cheche nyingine naziona katika majimbo mawili Mwanza, mkoani Mara yapo majimbo matatu hadi manne ambayo wagombea wa chama tawala wasikose Panadol mkononi siku ya kupiga kura. Dodoma kwa mara ya kwanza nako kuna jimbo lipo hatarini. Arusha, Mbeya, Kilimanjaro, Mtwara na Iringa, nako kuna majimbo yana cheche.

Sitanii, yote hayo yanaweza kutokea ila katika uchaguzi huu tunatarajia kusikia sera, si matusi kwa wagombea. Sitarajii kukuta watu wanaparurana kwa nafasi badala ya kutueleza wakichaguliwa watalifanyia nini taifa letu. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa CHADEMA kutoshiriki uchaguzi huu, shamrashamra hazitakuwa nyingi. Ni haki yao kufanya uamuzi walioufanya, ila ni wazi uamuzi huu umeumiza wanachama wao wengi. Zamu hii CHADEMA ilikuwa na nafasi ya wazi ya kushinda angalau viti 40 vya ubunge. Udiwani ndiyo usiseme. Maji yakiishamwagika…
Kwa upande wa CCM wamefanya mabadiliko. Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, akichukua nafasi ya Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi aliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dk. Samia.
Hii ni historia nyingine, kwani chama hiki hakikuwahi kupata Katibu Mkuu mwanamke. Hongera sana Dk. Migiro. Hongera pia Kenan Kihongosi kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM. Naamini usukani uliokabidhiwa Dk. Migiro utaendelea kuitendea haki Tanzania kwa kuzidi kuonyesha uongozi bora. Hongereni sana.




0784 404 827