Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Dkt. Asha-Rose Migiro amepokelewa rasmi katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)akiwa Katibu Mkuu huku akimefungua ukurasa mpya katika historia yake ya uongozi kwa kuwa Katibu Mkuu mpya Mwanamke.

Ikumbukwe kuwa tangu kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, nafasi hiyo kwa mara ya kwanza inashikiliwa na mwanamke.

Uteuzi huu si tu wa kihistoria bali pia ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa usawa wa kijinsia katika nafasi za juu za uongozi nchini Tanzania.

Akizungumza jijini Dodoma leo Agosti 26,2025 mara baada ya kupokelewa rasmi katika Makao Makuu ya CCM, Dkt. Migiro ametoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa Chama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo muhimu.

Ameeleza kuwa uteuzi huo ni heshima kubwa lakini pia ni dhamana ya kuendeleza misingi ya chama kwa weledi, uadilifu na moyo wa uzalendo.

Amesisitiza kuwa yuko tayari kutumikia chama kwa nguvu zote, huku akiwataka wanachama kushikamana kuhakikisha CCM inaibuka na ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025.

Dkt. Migiro, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa, anatambuliwa kama miongoni mwa viongozi wanawake waliowahi kuiwakilisha Tanzania kwa hadhi ya juu kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Waziri wa Sheria na Katiba, na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Uzoefu wake unatazamwa kama rasilimali kubwa kwa chama katika kipindi hiki kinachohitaji uimara wa kisiasa na uongozi wa kiutu na kimaono.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemtaja Dkt. Migiro kama kiongozi mwenye maono, busara na uelewa mpana wa siasa na utawala. Dkt. Nchimbi, ambaye sasa ni mgombea mwenza wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Mwenyekiti wa Chama kwa kumuamini wakati wa uongozi wake, pamoja na wanachama wa CCM kwa ushirikiano waliomuonesha.

Katika historia yake ya zaidi ya miongo minne, CCM imeongozwa na makatibu wakuu wanaume pekee, kuanzia Mzee Pius Msekwa hadi Dkt. Nchimbi.

Kwa uteuzi huu, Dkt. Migiro ameweka alama mpya, akifungua milango zaidi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi wa chama na taifa.

Uamuzi huu unaweka sura mpya ya uongozi ndani ya CCM kwa mara ya kwanza, chama kinakuwa na Mwenyekiti mwanamke na Katibu Mkuu mwanamke kwa wakati mmoja hatua inayozidi kuonesha kuwa Tanzania inaendelea kusonga mbele katika kujenga mfumo wa kisiasa jumuishi, unaotambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.