Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Miongoni mwa mambo yaliyoipa CCM uhai, uimara na uimarikaji katika safari yake ndefu ya kisiasa, ni hekima ya kuwatumia viongozi wakuu wastaafu kama washauri. Utaratibu huu si jambo jipya, bali ni urithi ulioanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mara tu baada ya kustaafu kwake kutoka nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM.

Tangu wakati huo, busara ya viongozi waliostaafu imekuwa nguzo ya kuimarisha chama, kulinda mshikamano wa kitaifa na kuhakikisha kuwa mwendelezo wa fikra na falsafa za uongozi haukatiki.

Safari ya Utaratibu Huu

Awali, viongozi wakuu wastaafu waliteuliwa kuwa Wajumbe waalikwa wa kudumu katika vikao vya juu vya Chama—yaani Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Hii iliwapa fursa ya moja kwa moja kushiriki kwenye maamuzi makubwa ya chama baada ya kustaafu, huku wakiendelea kulisaidia Taifa kwa hekima na uzoefu wao.

Ndivyo ilivyokuwa kwa viongozi wakuu kama Mwalimu Nyerere, Rais Ali Hassan Mwinyi, na Rais Benjamin William Mkapa baada ya kumaliza muda wao wa uongozi.

Mageuzi Wakati wa Rais Kikwete

Mageuzi muhimu yalijitokeza katika uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye akiwa Mwenyekiti wa CCM aliona umuhimu wa kupanua wigo wa ushirikishwaji. Ilipendekezwa kuwa hata Marais Wastaafu wa Zanzibar, ambao pia walihudumu kama Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, pamoja na Makamu Wenyeviti wengine wastaafu, washirikishwe rasmi.

Hapo ndipo likazaliwa wazo la kuunda Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu.

Muundo na Hadhi ya Baraza

Baraza hili la kipekee linaundwa na: Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao pia ni Wenyeviti Wastaafu wa CCM, Marais Wastaafu wa Zanzibar, ambao pia ni Makamu Wenyeviti Wastaafu wa CCM, pamoja na Makamu Wenyeviti Wastaafu wengine wa CCM.

Kwa kuundwa kwa baraza hili, viongozi hao wakaacha rasmi kuwa Wajumbe waalikwa wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na badala yake wakawa chombo maalum cha kushauri, kusikilizwa na kuheshimiwa.

Nguvu ya Busara na Mwendelezo

Hadi sasa, Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu limeendelea kuwa jukwaa muhimu la mshikamano wa kitaifa, hekima na ushauri thabiti. Ni baraza linalojumuisha kumbukumbu ya kihistoria, uzoefu wa uongozi na uadilifu uliojengwa kwa miongo kadhaa ya utumishi kwa Taifa.

Kupitia baraza hili, CCM imeendelea kuthibitisha kuwa chama makini ni kile kinachothamini hekima za wazee na kuunganisha kizazi kilichopita na kizazi kilichopo. Hii ndiyo sababu CCM imeendelea kuwa chama chenye uimara, mshikamano na uwezo wa kusimama kama nguzo kuu ya kisiasa nchini Tanzania.

Kwa hakika, Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu ni kiashirio cha heshima, mshikamano na busara za kisiasa zinazolinda ustawi wa Taifa letu na uthabiti wa Chama Cha Mapinduzi.