Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu
Shughuli katika miji midogo kadhaa iliyopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi zilisimama kwa muda wakati mteule wa kugpmbea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa, alipochukua fomu.
Masanja Kungu Kadogosa, mteule wa CCM Bariadi Vijijini, amechukua fomu na anatarajia kuzirejesha Agosti 27, 2025 kusubiri baraka za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC); takriban miezi miwili tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

“Kampeni zitakapoanza, tutapita kuwaambia namna gani tutakavyotekeleza Ilani ya CCM 2025/30. Bariadi itakuwa kama Ulaya,” anasema Kadogosa akishangiliwa na wananchi na wanaCCM kijijini Dutwa, Bariadi mkoani Simiyu.
Kadogosa ni mzaliwa wa Dutwa mwenye shahada ya uzamili (Masters in Accounting and Finance) kutoka Chuo Kikuu cha Gothenburg kilichopo nchini Sweden.
Awali, akisindikizwa na mamia ya wanachama wa CCM wenye nyuso za bashasha, Kadogosa akiwa ameshikilia kifimbo kama kile cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alifika ofisi za Halmashauri ya Bariadi Vijijini kuchukua fomu.

Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo jipya, Beatrice Gwamagobe, ndiye aliyemkabidhi fomu hizo, kisha kufuatiwa na maandamano yaliyoambatana na kila aina ya burudani.
“…tukishapitishwa na INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), wakisema huyu tumemkubali, ndipo tutaanza kupita rasmi,” anasema Kadogosa akishangiliwa na wananchi.
Anawakumbusha wananchi kwamba kampeni zitazinduliwa rasmi Agosti 28, 2025 na kwamba kazi waliyonayo ni moja tu; kueleza CCM imefanya nini katika walichokiahidi mwaka 2020.
“Na tutaeleza nini tuatarajia kufanya mwaka 2025/30. Wakati sisi tukipita, pia mgombea wetu wa Urais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi nao watapita,” anasema huku akichombeza kwa lugha ya Kisukuma katika harakati za kuweka msisitizo wa kile anachokizungumza.

