Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, ameishukuru Kamati Kuu ya chama hicho kwa heshima ya kumteua kushika nafasi hiyo, akiahidi kushirikiana na viongozi wenzake kuendeleza uimara wa chama hicho kikongwe nchini.
Akizungumza Agosti 26,2025 katika Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma, mara baada ya mapokezi yake, Dkt. Migiro na kukabidhiwa ofisi ameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wanachama na wananchi waliomlaki, akibainisha kuwa mshikamano huo ni ishara ya ushindi wa chama katika chaguzi zijazo. Aidha, alimpongeza mtangulizi wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa uongozi aliouonesha na kwa namna alivyoshirikiana na sekretarieti na kamati mbalimbali za chama katika utekelezaji wa majukumu.
Kwa upande wake, Dkt. Nchimbi alitumia fursa hiyo kumshukuru Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani na nafasi aliyompa ya kulitumikia chama katika kipindi chake cha uongozi. Alisisitiza ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu na yupo tayari kutekeleza majukumu yoyote atakayokabidhiwa na chama.
Aidha, alimwelezea Dkt. Migiro kama kiongozi mwenye weledi, uzoefu wa kitaifa na kimataifa, na sifa zinazompa nafasi ya kuliongoza chama kwa ufanisi. “CCM ipo kwenye mikono salama kwa kuwa Dkt. Migiro ni kiongozi mwenye uthubutu na uadilifu,” amesema
Dkt. Nchimbi ameacha kumbukumbu ya uongozi ndani ya chama, safari yake ya kisiasa ikianzia akiwa kijana na kupanda ngazi mbalimbali hadi kufikia nafasi ya Katibu Mkuu na sasa ni mgombea mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara.



