-Asema Nyasa bila utapiamlo, udumavu, upungufu wa damu inawezekana

-Wajawazito wahimizwa kutumia madini Chuma

-Atoa rai kwa Wataalam wa Afya kuzingatia Weledi,ushirikiano kupata Matokeo

Na Byarugaba Innocent, Nyasa DC

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe.Peres Magiri ametoa wito kwa wananchi kutambua umuhimu wa lishe Bora kwa afya ya mwili wa binadamu kwani ni Msingi wa mambo mengi ikiwemo kufanyakazi na kufikiri sawasawa.

Mhe.Magiri ameyasema hayo wakati wa kikao cha tathimini ya lishe kilichofanyika mwanzoni mwa juma kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kikiangazia umuhimu wa lishe,Mikakati na utekelezaji wake.

Akisoma taarifa ya tathimini na utekelezaji wa Mkataba wa lishe kwa kipindi cha Mwezi Aprili-Juni,2025 Afisa lishe Wilaya Teddy Mukama amesema hali ya lishe shuleni imeendelea kuimarika ukilinganisha na kipindi kilichopita kwani Watoto 54,424 kati ya 57,509 sawa na 94.64% wanapata chakula

Mukama ameongeza kuwa Wilaya inatambua kuwa lishe Bora ni Msingi wa Maendeleo kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa kwa ujumla hali ambayo hulifanya Taifa kuwa na Maendeleo katika nyanja za Kiafya, Kiakili na kiuchumi

Aidha,Mukama amesema kuwa katika kipindi cha Aprili-Juni kulikuwa na Watoto 5221 waliohitaji kunyonyeshwa maziwa ya Mama,wajawazito 6027 waliohitaji kupata madini Chuma hivyo kutokana na uhamasishaji kutoka kwa wataalam,Watoto na wajawazito wote wamepata huduma stahiki kwa 100%

Kwa upande mwingine Mukama ameeleza kuwa Mkakati wa Wilaya ni kuwa na watu wenye afya njema hiyo Watoto 94 kati ya 1191 sawa 7.89% wenye uzito pungufu,Watoto 2 kati ya 13,428 wenye utapiamlo Mkali na wajawazito 6 kati ya 1653 ambayo ni 0.4% wenye upungufu wa damu watawekwa kwenye programu Maalum kuwaimarisha.

Mhe.Magiri amewapongeza Watalaam wa Sekta ya afya,lishe na Watendaji wa Kata kwa kazi nzuri ya uhamasishaji kwani tathimini inaonesha Maendeleo chanya.
“..Naamini tunakwenda vizuri,nataka nione tukipiga hatua kwenye utekelezaji wa afua za lishe kama Wilaya. Nasisitiza uaminifu na uadilifu kwenye kujaza taarifa ili tuweze kupata Matokeo ya kweli yatakayorahisisha ufanyaji wa maamuzi kufanikisha afua za lishe ” ameongeza Mhe.Magiri

Katibu tawala Wilaya ya Nyasa Salumu Ismail amempongeza Afisa lishe Wilaya Teddy Mukama kwa jutihada za kupita vijijini kuhamasisha unyonyeshaji salama sambamba na kuanzisha klabu za lishe shuleni.

“Huu ni uwekezaji Mkubwa.Watoto hawa ni Wazazi wa baadaye,haya wanayojifunza watayatumia baadaye kwenye maisha na kuleta tija kwa Taifa katika kupambana na udumavu” amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Khalid A.Khalif amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa Nyasa itaendelea kupiga hatua katika Mkataba wa lishe kwani Wataalam wanatambua kuwa Taifa lisilokuwaa na watu wenye lishe Bora halitakuwa na wazalishaji.