๐Ÿ“Œ Ni kwa mara ya kwanza kufanyika Afrika Mashariki na Kati

๐Ÿ“Œ Aipa kongole Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 kwa wagonjwa 50 wa kwanza

๐Ÿ“Œ Asema Serikali itaendelea kuweka msukumo ushirikiano na Sekta binafsi

๐Ÿ“Œ Awaasa Watendaji Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza pale Sekta binafsi inapofanya vizuri

๐Ÿ“Œ Wagonjwa 300 wanufaika na teknolojia ya utoaji uvimbe bila upasuaji

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameziindua teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayofahamika kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki ikiwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Akizindua huduma hiyo Agosti 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko amepongeza Watendaji wa hospitali ya Kairuki pamoja na muasisi wake Hubert Kairuki na Mkewe kwa uthubutu wao katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma hiyo ya HIFU ambayo imeiweka Tanzania katika rekodi ya kutoa uvimbe bila kufanya upasuaji barani Afrika suala ambalo pia litaongezea nchi mapato.

Ameeleza kuwa awali huduma ya HIFU barani Afrika likuwa ikipatikana katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.

Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 la gharama za matibabu ya utoaji uvimbe bila upasuaji kwa wagonjwa 50 wa kwanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo ikiwa ni kielelezo cha Watendaji wa hospitali hiyo kuonesha utu kwa Watanzania, kuacha alama njema na kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kutoa huduma kwa watanzania kwa gharama nafuu.

Dkt. Biteko amesema kuwa kufanyika kwa tukio hilo muhimu ni kielelezo cha Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa msukumo sekta binafsi na kuikuza ili kutoa huduma za matibabu kwa wananchi kwa ufanisi na kusogeza karibu huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani ndani ya nchi hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono Sekta binafsi.

ยทAidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kuanzisha Idara ya huduma za dharura ambayo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9,000 kwa mwaka.

Katika hatua, nyingine, Dkt. Biteko amewataka Watendaji katika Wizara ya Afya kutoogopa kujifunza kutoka Sekta binafsi pale inapofanya vizuri na wawape ushirikiano wakati wote siyo nyakati za ukaguzi tu kwani lengo la Serikali ni kufikisha huduma bora kwa wananchi kwa ushirikiano wa Serikali na sekta hiyo.

Kuhusu ombi la Hospitali ya Kairuki la kujengewa barabara ya lami ya mita 300 kuelekea kwenye hospitali hiyo ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi ameelekeza Manispaa ya Kinondoni kufanyia kazi ombi hilo.

Dkt. Mwinyikondo Amir, kutoka Wizara ya Afya akimwakilisha Waziri wa Afya, amesema kuwa tukio hilo ni ishara ya ushirikiano uliopo kati ya sekta binafsi na Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema Wizara ya Afya imekuwa na ushirikiano mkubwa na Hospitali ya Kairuki katika masuala mengi ikiwemo matumizi ya Bima ya Afya na kwamba pande zote mbili zinatambua kuwa zina wajibu wa kutekeleza dira ya maendeleo ya 2050 inayoelekeza uwepo wa jamii yenye afya bora.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Afya na Elimu Kairuki, Kokushubila Kairuki ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema sekta ya afya imekuwa na maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba hospitali hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi hizo hasa ikiwa ni utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kujenga Taifa lenye uchumi imara na afya bora.

Amesema gharama za kuweka teknolojia hiyo ya HIFU ni shilingi Bilioni 12 na milioni 300.

Aidha amesema kutoka huduma ya HIFU ianze kutolewa tayari wananchi 300 wamepata huduma za uchunguzi huku 298 wakipata matibabu.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kairuki,
Dk. Onesmo Kaganda alisema uzinduzi wa HIFU ni tukio la kihistoria kwakuwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Amesema teknolojia hiyo barani Afrika imeanzishwa katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.

Ameeleza kuwa HIFU ni Teknolojia ya kisasa inayotumia Mawimbi Sauti (Sound Waves) b kutibu aina mbalimbali za uvimbe mwilini bila upasuaji, ikiwemo uvimbe wa saratani na usiokuwa wa saratani katika maeneo kama Matiti, Kongosho, Kizazi kwa Wanawake, na Tezi Dume kwa wanaume.

Ameeleza faida za huduma hiyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na kovu kwa kuwa hakuna upasuaji, mgonjwa hawekewi nusu kaputi na mgonjwa hupona kwa muda mfupi na kurejea katika shughuli zake, matibabu hayahitaji kumwongezea damu mgonjwa hata kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu, pia kupunguza gharama za kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.

Ameongeza kuwa, faida nyingine ya HIFU ni pamoja na tiba shufaa ambayo husaidia dawa za saratani kufanyakazi vizuri mwilini, kufubaza kukua kwa saratani mwilini (slowdown disease progression) na kupunguza maumivu kwa wagonjwa wa saratani.

Amesema mtambo huo ulianza kufanya kazi desemba 2023 ambapo mpaka sasa wagonjwa 303 wamefanyiwa uchunguzi na 298 kupatiwa matibabu na kumekuwa na matokeo chanya ya wagonjwa hao.

Amesema kuwepo kwa teknolojia hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii Tiba Kusini mwa jangwa la Sahara.

Pia, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira wezeshi ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi Binafsi.

Kuhusu Idara ya Huduma za Dharura iliyozinduliwa katika Hospitali ya Kairuki amesema itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9000 kwa mwaka na pia imejizatiti kwa magonjwa ya dharura pindi yatakapotokea.