Mgombea ubunge wa Jimbo la Mafinga Mji kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ngwada Mubarak Twaha, ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ili kupambana na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana wenye shahada za vyuo vikuu ambao wamebaki kukosa mwelekeo licha ya elimu yao.
Alisema kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo atahakikisha changamoto ya ajira kwa vijana katika jimbo hilo linapungua kwa uanzishwaji wa miradi itakayosaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Alisema kuwa atahakikisha vijana wenye digrii wasio na ajira wanapata ajira za makusudi na za kudumu. Tunakwenda kuanzisha mfumo wa ajira unaotokana na miradi ya wananchi wenyewe na miradi hiyo itakuwa chanzo cha kodi na maendeleo kwa kila kata.
Alifafanua kuwa mpango wake unahusisha kuanzisha miradi mikubwa ya kiuchumi katika kata zote tisa za Mafinga Mji, ikiwa ni pamoja na kampuni za ujenzi, kampuni za ulinzi, viwanda vya mbao, shule binafsi za walimu, na studio za wasanii.
”Nitaimarisha michezo kwa kuanzishwa kwa timu za mpira wa miguu kila kata, zitakazounda timu ya jimbo itakayojulikana kama Mafinga Mji Shooting, ikishiriki ligi kubwa na hatimaye kupata uwanja wa kisasa utakaovutia mechi za Simba na Yanga” alisema.
