Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amejitokeza hadharani kuwajibu wanaodai kuwa utaratibu wa kumpata Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 haukufuata taratibu, akiwataka waache kupotosha umma na kuonesha wazi kuwa wanajitoa ufahamu.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe – Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM, Dkt. Jakaya Kikwete alisema utaratibu uliotumika kumpitisha Rais Samia ndio huo huo uliotumika kwa marais waliopita tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi.
“CCM imekuwa na utaratibu wa kumpata mgombea Urais tangu enzi za Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, mimi mwenyewe, Hayati Dkt. John Magufuli, na sasa Dkt. Samia. Utaratibu ni uleule – Mkutano Mkuu kupitisha jina lililowasilishwa. Sasa mbona huko nyuma hawakupinga, leo ndio kelele zinatokea?” alihoji Kikwete huku akishangiliwa na wafuasi wa chama.
Amesisitiza kuwa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18 na 19, 2025, ndio ulioidhinisha jina la Dkt. Samia kwa mujibu wa Katiba na taratibu za chama, na kwamba yeye binafsi anauunga mkono kikamilifu mchakato huo.
Kikwete aliongeza kuwa madai ya kupinga utaratibu huo hayana mashiko kwa sababu hata wale wanaolalamika leo walikuwepo katika awamu zote zilizopita, lakini hawakuwahi kusema chochote.
“Watu wanaosema hayo walikuwepo tangu enzi za Mkapa hadi Magufuli. Wamekaa kimya huko nyuma, lakini leo wanakuja na maneno ya kupotosha. Hii ni kuonesha wazi kuwa si hoja ya kweli bali ni kujitoa ufahamu,” alisema.
Rais Mstaafu huyo alitumia pia nafasi hiyo kueleza kwanini kauli ya “Mitano Tena kwa Samia” imeibuka, akisema inatokana na kazi kubwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020–2025 pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Rais Samia aliikuta na kuibeba ipasavyo licha ya changamoto zilizokuwepo baada ya kufariki kwa Hayati Magufuli.
Kwa mujibu wake, Dkt. Samia amethibitisha umahiri wake katika uongozi, ameendeleza amani na mshikamano wa taifa, na ameonyesha uwezo mkubwa wa kusimamia uchumi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
“Alipoingia madarakani kulikuwa na hofu kama ataweza kubeba miradi mizito iliyokuwepo, lakini ameuthibitishia umma uwezo wake. Leo tumekutana tena kumuunga mkono ili apate ridhaa ya kuongoza Tanzania kwa miaka mingine mitano,” alisisitiza Kikwete.
Uzinduzi wa kampeni hizo pia ulijumuisha utambulisho wa mgombea mwenza wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, huku maelfu ya wafuasi wakishuhudia tukio hilo kubwa linalozindua rasmi mbio za uchaguzi kwa chama hicho tawala.

