Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Taifa la Elimu na Ufundi Stadi (NACTVET), limezipatia Ithibati Program mpya tano za Chuo cha Elimu ya Biashara CBE kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kuanzishwa kwa program hizo ni sehemu ya jitihada za Chuo hicho katika kuhakikisha wanatoa elimu bora, ya kisasa na inayoendana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Alisema wameanzisha Shahada ya Usimamizi wa Biashara (Double Degree) ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaRais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Agosti mwaka jana wakati wa katika kikao chake pamoja na Hazina na Viongozi wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Uma ya kuwekeza nje ya Nchi.

“ Chuo chetu kimeanzisha program hii inayolenga kuwaandaa wanafunzi kuwa mameneja na viongozi bora katika taasisi za umma na binafsi. Programu hii itawawezesha wahitimu kupata ujuzi wa kupanga, kuongoza na kusimamia biashara za ndani na za kimataifa kwa ufanisi,” alisema na kuongeza

“ Faida yake kubwa ni kuongeza idadi ya wataalamu wa usimamizi wa biashara watakaosaidia kukuza Uchumi wa Taifa. Program hii inatolewa kwa ushirikiano wa CBE na Chuo cha Southern West University of Finance and Economics (SWUFE) kutoka China ambapo makubaliano yameshasainiwa,” alisema.

“ Program hii ya Double Degree ni program ya kwanza kutolewa hapa nchini kwa mtindo wa Double Degree ambapo mwanafunzi atasoma miaka miwili Tanzania na miaka miwili atasoma nchini China,” alisema.

Aliongeza kuwa wameanzisha Shahada ya digital technologies katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kupata wahitimu wenye uwezo wa kutatua changamoto zinalolikabili Taifa zikiwemo za kiteknolojia, kiuchumi na ukosefu wa ajira kwa vijana.

Profesa Mganilwa alisema chuo kimeanzisha program hiyo ya kipekee inayolenga kutumia Teknolojia za Kidijitali kuleta suluhisho la changamoto ambapo itafundishwa sambamba na mfumo wa mafunzo kwa vitendo/ Uanagenzi (Apprenticeship).

“Wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza darasani Semesta moja na Semesta nyingine watajifunza kwa vitendo katika mazingira ya kazi. Faida yake kubwa ni kuwaandaa vijana kuwa wataalamu wa teknolojia, na suluhisho za kidijitali, jambo ambalo ni muhimu sana katika karne ya Sayansi na Teknolojia. Program hii itaendeshwa kwa ushirikiano wa CBE na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambapo makubaliano yameshasainiwa.

Alisema katika kuunga mkono Sera Mpya ya Elimu iliyopitishwa na Serikali hivi karibuni, CBE imeanzisha program ya Shahada ya uchumi na Uhasibu inayolenga kuzalisha walimu wa shule za Sekondari wenye utaalamu wa uhasibu na Uchumi kwa kuzingatia Sera mpya ya Elimu.

“ Faida yake ni kuimarisha uwezo wa kufundisha masomo ya Uhasibu na Uchumi katika shule za Sekondari, hivyo kuongeza ubora wa elimu ya sekondari kwa kuzalisha wahitimu wa kutosha wanahitajika kwa wingi kutokana na mahitaji yaliyotokana na kuanzishwa kwa Sera ya Elimu Mpya,” alisema.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, aliwataka vijana kuchangamkia program hizo ili kupata maarifa yatakayowawezesha kukidhi vigezo vya kupata ajira ndani na nje ya nchi.